BAADHI ya ng’ombe katika kijiji cha Arash Loliondo, Ngorongoro, mkoani Arusha, wameshindwa kupata soko kutokana na kuwa na majeraha ya risasi huku wengine wakiendelea kuishi na risasi hizo mwilini, anaandika Nasra Abdallah.
Ng’ombe hao walipigwa risasi wakati wa operesheni ya kuwaondoa mifugo iliyofanywa na Mamlaka za Hifadhi kwa lengo la kutaka kumega eneo la kilometa 1500 katika vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Serengeti na kupafanya pori tengefu.
Timu ya waandishi ambayo ilifika katika vijiji vilivyoathiriwa na zoezi hilo kwa lengo la kujionea athari za kiuchumi zilizotokana na operesheni hiyo, ilielezwa kwamba kwa sasa kumekuwa na umasikini wa hali ya juu kutokana na ukweli kwamba uchumi mkubwa wanaoutegemea wakazi wa maeneo hayo ni mifugo.
Mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Ngostelo Lilash, amesema awali kabla ya operesheni waliweza kuuza ng’ombe mmoja hadi Sh. milioni moja, lakini kutokana na mifugo hiyo kwa sasa kuwa na majeraha ya risasi na wengine kuwa wadhoofu kutokana na ukame wameshuka bei hadi Sh. 400,000.
Naye Kutare Kumari, amesema wamekuwa wakilazimika kumlipa daktari kwa kutibu ng’ombe mmoja kwa Sh. 50,000 kila siku na hivyo ng’ombe mmoja kuwagharimu Sh. 350,000 kwa wiki.
Kama vile haitoshi amesema mpaka sasa wananuka madeni ya kukopa kwa riba ili kuweza kiwakomboa ng’ombe wao waliokamatwa kipindi cha operesheni hali inayowafanya maisha yao kuzidi kuwa magumu.
“Mbali na kukopa fedha pia tunalazimika wakati mwingine kuuza kondoo kwa hasara ili kuweza kukomboa ng’ombe wetu ambapo mpaka sasa timeshatumia zaidi ya milioni kumi katika shughuli hiyo na bado tunadaiwa fedha,” amesema Kumari.
Wito wao kwa serikali, wakazi hao waliomba serikali iwape mifugo yao kwa kuwa ilikamatwa nje ya hifadhi na kuongeza kuwa ni vema idara ya mifugo katika Halamshauri ya Ngorongoro kuwapelekea madaktari wa mifugo.
Leave a comment