Saturday , 4 May 2024
Home Kitengo Biashara RC Chalamila azindua NMB Onja Unogewe, aiita akili kubwa
Biashara

RC Chalamila azindua NMB Onja Unogewe, aiita akili kubwa

Spread the love

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila ameipongeza Benki ya NMB  kwa kuzindua huduma mpya chini ya Mwamvuli wa Teleza Kidigitali iitwayo ‘NMB Onja Unogewe’ kwa kuwa ni muarobaini wa upotevu wa pesa, uporaji, wizi, matumizi yasiyo ya lazima na hatarishi nyinginezo zitokanazo na matumizi ya pesa taslimu. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Chalamila, ameitaja huduma hiyo kuwa ni zao la akili kubwa na ubunifu wa wafanyakazi wa benki hiyo, unaoenda kuihakikishia jamii njia rahisi na salama ya kupokea fedha na kufanya malipo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila (wapili kushoto) akiskani QR maalum kuashiria uzinduzi wa kampeni maalum ya Onja unogewe ya Benki ya NMB katika viwanja vya kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam. Kampeni hii inalenga kuhamasisha wateja kutumia zaidi malipo kwa njia ya kuskani QR za NMB (Lipa Mkononi). Kulia ni Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, watatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Kushoto ni Mkuu wa Idara ya kadi wa Benki ya NMB, Philbert Casmir.

Sambamba na hayo, RC Chalamila ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi uliofanyika Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam, alisema NMB Onja Unogewe ni huduma chanya iliyovuka mstari wa huduma za kibenki na kwamba Serikali inaitarajia itaenda kuwa chachu ya kukuza elimu ya uhifadhi na matumizi sahihi ya fedha kwa Watanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Chalamila alisema Serikali inapongeza ubunifu wa suluhishi za kifedha unaofanywa na NMB.

“Mtaji mkubwa wa NMB tangu ilipoanzishwa (1997) hadi sasa inapokuwa kinara wa huduma za kifedha nchini, ni watumishi wabunifu, walio na akili kubwa za kufikiria suluhishi sahihi, rahisi, nafuu na salama za kifedha kama hizi. Kwa miaka yote hiyo, benki ‘imeji-transform’ yenyewe na hiyo kuwa chachu ya kupaa kwao kimafanikio.

“Kuna matarajio makubwa ya kufanya vizuri mara 20 ya ilivyo sasa katika miaka kadhaa ijayo, kwa sababu NMB inaziona changamoto zitokanazo na matumizi ya pesa taslimu kuwa ni fursa, ikaja na suluhishi hizi hizi za kidigitali kusaidia jamii kuachana na utamaduni wa matumizi yasiyo sahihi na kuongeza uhifadhi wa fedha zao,” alisema RC Chalamila.

Aliwataka watoa huduma mbalimbali za kijamii wakiwemo waendesha bodaboda, bajaji, mama lishe, wauza maduka, wafanyabiashara na wajasiriamali wa kada zote jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa ya NMB Onja Unogewe kwa kupata QR Code zao na kuzitumia kwa ustawi na ukuaji wao kiuchumi.

“Achaneni na utamaduni wa kutunza fedha kwenye vibubu majumbani ama kuweka madukani, ambako hatari za upotevu, wizi ama ajali za matukio ya kuunguliwa moto ni nyingi, kimbilieni katika suluhishi hizi matawini, chukueni QR Code zenu na mfanye malipo kupitia hizo kwa usalama wa pesa za mtu mmoja mmoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisisitiza.

Awali, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema benki yake inajivunia sana bunifu za suluhishi za kifedha, alizozitaja kuwa ni siri ya mafanikio ya benki hiyo, ambayo mwaka jana uliuongezea thamani Mwamvuli wa Teleza Kidigitali ulioanzishwa mwaka 2019 kwa kuizindulia Huduma ya NMB Pesa Wakala – huduma maalum ya kuweka na kutoa pesa kirahisi kupitia mawakala wanaotumia simu za mkononi.

“NMB Onja Unogewe ni maboresho ya Huduma ya Lipa Mkononi ‘QR Code,’ ambayo yanaenda kumpa wigo mpana mteja wa kulipia huduma kwa njia ya kidigitali, ambako atanufaika na rejesho la asilimia 10 katika malipo yake.    Tunafanya hivyo kwa makusudi ili kuvutia zaidi watumiaji wa huduma zetu za kimtandao ili kupunguza matumizi ya pesa taslimu.

“Pamoja na suluhishi hizi zote tunazobuni, kuzindua na kutoa kwa Watanzania, bado tunao utamaduni endelevu wa kurejesha kwa jamii katika sekta za elimu, afya na mazingira.

“Tayari tumepanda miti 500,000 kupitia Kampeni Endelevu ya Upandaji Miti Milioni 1 mwaka huu wa 2022, pamoja na misaada kwenye mashule na hata Hospitali zetu, ikiwemo ya Taifa ya Muhimbili ambako tumeingia makubaliano ya kuboresha Wodi ya Uzazi na tumetumia zaidi ya Sh. Mil. 250,” alibainisha na kusema Dar wametumia zaidi ya Mil. 80 katika elimu.

Kwa niaba ya NMB, Mponzi aliahidi kwamba benki hiyo itaendelea kuwa bega kwa bega na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua kero na changamoto zinazokwaza ustawi wa elimu na huduma za afya nchini, huku akiwataka watoa huduma za bodaboda, bajaji, mama lishe, wauza maduka, wafanyabiashara na wajasiriamali kufika matawini kupata QR Code zao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Biashara

Cash Days Promo mamilioni yanakusubiri, cheza kupitia Meridianbet kasino 

Spread the love  JIANDAE kwa mshangao wa kustaajabisha Meridianbet kasino ya mtandaoni...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yazindua huduma maalum kwa wastaafu

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua huduma maalum kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yazindua akaunti ya Kikundi

Spread the loveBenki ya NMB imezindua akaunti ya kikundi yenye  maboresho makubwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyakazi waidai STAMICO mishahara ya bilioni 1

Spread the loveWALIOKUWA wafanyakazi wa mgodi wa Shirika la Madini la Taifa...

error: Content is protected !!