May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atoa tahadhari wimbi la tatu la Covid-19

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya mlipuko wa tatu wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia ametoa wito huo leo Ijumaa, tarehe 25 Juni 2021, akizungumza na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini mkoani Dar es Salaam.

Kiongozi huyo wa Tanzania, amesema kuna ishara zinazoonesha wimbi hilo la tatu limeingia nchini na kwamba tayari kuna watu wameshaathirika na ugonjwa huo.

“Kama tunavyojua duniani kuna wimbi la tatu la Corona, tumetoka la kwanza sasa tumeingia la pili. Limepungua kidogo na sasa kuna la tatu, ishara ndani ya nchi inaonekana tayari tuna wagonjwa wameonekana wa wimbi la tatu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema, alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, tarehe 1 Juni 2021, alibaini kuna wodi ilikuwa na wagonjwa wa Covid-19.

“Kama mnamkumbuka kuna siku nilitembelea Mwanayamala, kuna wodi daktari mfawidhi alikuwa ananiingiza, akanaimbia humu kuna wagonjwa wenye matatizo ya kupumua. Nikamuambia kuwa muwazi ni Covid-19? Akasema ndiyo Covid-19,” amesema Rais Samia.

Akielezea mkasa huo, Rais Samia amesema “wakati wapiga picha wangu wameshatangulia, nikawaambia tokeni haraka. Ni kusema hili jambo bado lipo tusiliache, tuchukue tahadhari zote.”

Rais Samia amewaomba viongozi wa dini, kuendelea kuwahimiza waumini wake kufuata miongozo inayotolewa na wataalamu, kuhusu kujikinga na ugonjwa huo.

“Nafahamu kanisa tangu mwanzo limekuwa na msimamo thabiti wa kupambana na ugonjwa huu, niwaombe maaskofu na viongozi wengine wa dini, pamoja na masuala mengine tunayohubiri msisahau kuwakumbusha waumini kuhusu kujikinga na kuchukua tahadhari zinazoelekezwa na wataalamu wa afya dhidi ya maambukizi ya Corona,” amesema Rais Samia.

Rais wa TEC, Askofu Mkuu, Gervas Nyaisonga

Awali, Rais wa TEC, Askofu Mkuu, Gervas Nyaisonga, alimpongeza Rais Samia kwa hatua alizochukua katika kukabiliana na maambukizi ya Covid-19.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Rais Samia kukabiliana na ugonjwa huo, ni uundwaji wa tume ya wataalamu kwa ajili ya kufanya tathimini ya mwenendo wa Covid-19 nchini.

Timu hiyo aliiunda kipindi kifupi baada ya kuingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, kufuatia kifo cha aliyekuwa mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi mwaka huu, kwenye Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.

Kwa mara ya kwanza Tanzania iliripoti kisa chake cha kwanza cha Covid-19, Machi 2020.

error: Content is protected !!