May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ateua mwenyekiti mpya NEC

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameteua viongozi mbalimbali, akiwemo Jaji Jacob Casthom Mwambegele, aliyemteua kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya uteuzi huo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 27 Desemba 2021 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Jaffar Haniu.

Taarifa ya Haniu imesema, Jaji Mwambegele anachukua nafasi ya Jaji Mstaafu Semistocle Kaijage, aliyemaliza muda wake.

“Rais Samia amefanya uteuzi wa viongozi wafuatao, amemteua Jaji Mwambegele kuwa Mwenyekiti wa NEC. Jaji Mwambeele ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na mjumbe wa NEC, anachukua nafasi ya Jaji Kaijage ambaye amemaliza muda wake,” imesema taarifa ya Haniu.

Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage

Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Jaji Mwanaisha Athuman Kwariko, kuwa Mjumbe wa NEC, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mwambegele.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Jaji wa Mahakama Kuu, Sam Mpaya Rumanyika, kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Pia, Rais Samia amemteua Profesa Khamisi Dihenga, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

“Prof. Dihenga anahudumu kwa mkataba katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Morogoro, anachukua nafasi ya Prof. William Anangisye, aliyemaliza muda wake,” imesema taarifa ya Haniu.

Taarifa ya Haniu imesema, Rais Samia amemteua Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Mussa Muhidin Kisaka, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

“Uteuzi huu umeanza tarehe 23 Desemba 2021,” imesema taarifa ya Haniu.

error: Content is protected !!