Spread the love

 

JESHI la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limeagiza Askofu wa Kanisa la Efatha, Josephat Mwingira, ahojiwe ndani ya saa 24 juu ya tuhuma anazodaiwa kuzitoa, dhidi ya Serikali. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Amri hiyo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 27 Desemba 2021 na Kamanda wa Jeshi la Polisi wa kanda hiyo, ACP Jumanne Muliro, saa chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kuliagiza jeshi hilo kumhoji Askofu Mwingira.

Ni baada ya hivi karibuni kiongozi huyo wa kiroho, kudai alinusurika kuuawa mara tatu na watu wa Serikali.

“Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es salaam, limeagiza ndani ya saa 24 kuanza kuhojiwa kwa Askofu Mwingira, juu ya tuhuma mbalimbali alizozitoa dhidi ya Serikali, ikiwemo njama za maofisa wa Serikali kutaka kumuua,” imesema taarifa ya Kamanda Muliro.

Kamanda Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo

Taarifa ya Kamanda Muliro imedai kuwa, kauli za Askofu Mwingira zinajenga chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali yao, hivyo watamhoji kwa kina katika vipengele watakavyoona vina viashiria vya kosa la jinai.

“Jeshi la Polisi limefikia hatua hiyo baada ya kufuatilia kwa karibu, kauli zinazodaiwa kutolewa na Askofu huyo na kuona kuwa zinajenga hofu na chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali yao,” imesema taarifa ya Kamanda Muliro na kuongeza:

“Kwa uzito wa mambo yanayodaiwa kutolewa na Askofu huyo, ni lazima apatikane haraka iwezekananyo na ahojiwe kwa kina juu ya kila kipengele ambacho Jeshi linaona kuna viashiria vya vigezo vya kijinai.”

Askofu Mwingira alitoa tuhuma hizo dhidi ya Serikali, akiongoza ibada kanisani kwake, iliyorushwa mbashara na Kituo cha Televisheni cha Star Tv, ambapo alidai alinusurika kuuawa mara tatu na watu wa Serikali.

Pia, alidai dada ambaye hakumtaja jina, alidai kuwa alimvujishia siri juu ya njama za yeye kuuawa, aliuliwa katika Hoteli ya Rombo iliyoko Shekilango, jijini Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *