December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Asilimia 88.9 wamechanja chanjo ya Corona

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema hadi kufikia jana tarehe 15 Oktoba, 2021 jumla ya Watanzania 940,507 walikuwa wamekwishachanja chanjo ya Covid – 19 sawa na asilimia 88.9 ya zaidi ya dozi milioni moja za chanjo aina ya Johnson & Johnson. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro …  (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Oktoba, 2021 katika ibada maalumu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Hospitali ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema Tanzania haina uhaba wa chanjo ya Uviko – 19 kwani chanjo ipo ya kutosha na chanjo nyingine ipo njiani inakuja.

“Lakini juzi tumepokea mzigo wa chanjo na mwingine upo njia unakuja kwa hiyo kwenye masuala ya chanjo hakuna mapungufu.

“Niendelee kuwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari zote kujipeusha na athari za ugonjwa wa Uviko-19 ikiwemo kuchanja pamoja na kufuata maelekezo ya wataalamu wetu, kwa kuwa hatujui huu ugonjwa utaisha lini,” amesema.

Aidha, amesema katika fedha Sh trilioni 1.3 za mkopo nafuu uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IFM) kwa Tanzania, jumla ya Sh bilioni tano zimetengwa kwa ajili ya utafiti.

“Ili kuwa na sekta ya afya yenye kujibu mahitaji ya wananchi, tafiti ni nguzo imara katika kukabiliana na mabadiliko ya magonjwa duniani, serikali imeendelea kufanya uwekeza mkubwa kupitia vyuo vikuu na taasisi za utafiti nchini KCMC ikiwa mojawapo. Niwapongeze kuendelea kufanya tafiti ikiwa wa UVIKO 19.

“Serikali imeendelea kutoa kipaumbele ambapo kupitia mkopo nilioutaja Sh bilioni 5.1 zimetengwa kuhakikisha taasisi mbalimbali zinazohusu Uviko 19, kuendelea kufanya tafiti ili kubaini njia rahisi ya kukabiliana nalo,” amesema.

Pamoja na mambo mengine alimuagiza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Molel kuhakikisha fedha za ujenzi wa jengo la mionzi tiba kwa wagonjwa wa saratani zinatolewa kwa wakati.

Amesema jengo hilo ambalo linagharamiwa na serikali  kwa asilimia 100 kwa gharama ya Sh bilioni nne, tayari Sh bilioni moja imekwishatolewa wakati Sh bilioni moja nyingine ipo kwenye mchakato wa kutolewa.

error: Content is protected !!