December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aeleza sababu uhaba watumishi wa afya, ataja ‘wages bill’

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema sababu ya kuwapo kwa uhaba wa watumishi wa kada ya afya na elimu ni kutokana na mahesabu ya ukuaji wa kiwango cha uchumi nchini. Anaripoti Mwandishi wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Oktoba, 2021 wakati akijibu changamoto zilizoibuliwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo katika ibada maalumu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Hospitali ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Dk. Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, amesema mojawapo ya changamoto tatu kubwa zinazoikabili hospitali hiyo ya KCMC ni upungufu wa watumishi wa afya katika ngazi zote.

Amesema katika ikama ya hospitali hiyo inatakiwa kuwa na watumishi 1634 lakini sasa wana upungufu wa watumishi 758 jambo ambalo linaathiri utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwani haijapewa kibali cha ajira kwa muda wa miaka minne sasa.

“Lakini pia changamoto nyingine ni muundo wa utumishi ‘Scheme of Services’, kutoidhinishwa na serikali ikilinganishwa na hospitali nyingine za rufaa

“Kutoidhinishwa kwa muundo wa utumishi wa hosptali ya KCMC umesababisha watumishi wetu kulipwa mishahara midogo ikilinganishwa na hospitali za kanda.

“Kwa mfano kada ya madaktari kuna tofauti ya Sh milioni 1,150,000, wauguzi wenye shahada Sh 972,959, wauguzi wenye stashahada Sh. 678,468,  Tunaomba hospitali ipitishiwe muundo wake wa utumishi kama ilivyopitishwa kwa hospitali nyingine za kanda,” amesema.

Dk. Shoo ameongeza kuwa changamoto nyingine ni ubovu wa barabara ya Stephano yenye urefu wa mita 850 ambayo inaingia hospitali hapo.

Aidha, akijibu changamoto hizo Rais Samia amesema anatambua upungufu huo wa watumishi lakini si kwa hospitali ya KCMC pekee.

“Hii ni kutokana na kiwango cha ukuaji wa uchumi, tunapopiga mahesabu ya uchumi kuna kitu kinaitwa ‘wage bill’, kwa hiyo hatuwezi kuvuka wage bill yetu kama serikali haiwezi kuvuka kiwango cha ukuaji wa uchumi.

“Kwa hiyo pale tunapopata upenyo uchumi ukikua kidogo, tunatoa ajira harakaraka hasa hizi zinazogusa maisha ya wananchi kama vile madaktari, wauguzi na walimu,” amesema.

Mbali na kusikitishwa kwamba kwa muda wa miaka minne hopsitali ya KCMC haikupata kibali cha kuajiri watumishi wapya, Rais Samia amemhakikishia Askofu Dk. Shoo kuwa atakapopata upenyo wa kuajiri atahakikisha KCMC inapata fungu la kuajiri japo si lote kwa kiwango kinachotakiwa.

Askofu Frederick Shoo, Mkuu wa Kanisa la KKKT

Akizungumzia kuhusu suala la changamoto ya muundo wa watumishi Rais Samia amesema atakwenda kuangalia vikwazo vilivyotokea na kuvifanyia kazi.

“Muundo huu ni muhimu kwani unaziweka sawa hospitali zetu na kuhakikisha watumishi wote wanapata stahili zao jinsi wanavyostahiki kulingana na majukumu yao,” amesema.

Kuhusu barabara Rais Samia amesema, kwa kuwa barabara haikuwepo kwenye mipango ya serikali, Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa watakwenda kukaa na kuangalia nani anatakiwa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

“Nikuhakikishie kwamba tutakiweka lami lakini si mwaka huu. Ubovu wa njia ni kero kwa wagonjwa wanaofuata huduma nasi tuko tayari kuondoa kero hiyo,” amesema.

error: Content is protected !!