RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amempendekeza Dk. Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Jina hilo, limewasilishwa bungeni leo Jumanne tarehe 30 Machi 2021 na mpambe wa Rais kisha Spika wa Bunge, Job Ndugai akalitangaza mbele ya Bunge.
Mara baada ya jina hilo kutangazwa, Dk. Mpango ambaye ni waziri wa fedha na mipango, alishikwa na butwaa huku kelele za kushangilia zikitawala bungeni huku mteuliwa mwenyewe, akiwa amekaa akiwa haamini.
Dk. Mpango aliyezaliwa Jumapili tarehe 14 Julai 1957, ni mbunge wa Buhigwe mkoani Kigoma, anachukua nafasi ya Samia, aliyeapishwa kuwa Rais kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli.

Dk. Magufuli, alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na mwili wake, kuzikwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita.
Dk. Mpango aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2015, baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kisha akateuliwa kuwa waziri wa fedha na mipango, nafasi aliyoitumikia mpaka leo Jumanne.
Katika uchaguzi mkuu ulipita wa mwaka 2020, Dk. Mpango alirejea nyumbani kwao, Buhingwe kugombea ubunge na kushinda.
Kuteuliwa huko kuwa makamu wa Rais, kunalifanya jimbo la Buhingwe kuwa wazi hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuitisha uchaguzi wa jimbo hilo.
Pia, nafasi ya waziri wa fedha na mipango nayo inakuwa wazi na Rais Samia atapaswa kuijaza.
Dk. Mpango, amewahi kuwa kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Leave a comment