Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amewaomba Wazanzibar wanaoishi nje ya nchi ‘Diaspora’, washirikiane na Serikali yake katika kuimarisha uchumi wa visiwa hivyo, kupitia utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Bluu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Mwinyi ametoa wito huo, leo Ijumaa, tarehe 31 Desemba 2021, akizungumza na Wazanzibar waishio nje ya nchi, kwa njia ya mtandao.

“Sera kubwa tuliyokuwa nayo ya uchumi wa bluu, lengo letu hizi sekta sita tunazozungumzia tuzipe kipaumbele kikubwa, tuzitafutie uwekezaji mkubwa ili tuweze kukuza uchumi wetu kwa haraka zaidi. Hapa inakuja nani wadau wa kushirikiana na Serikali, Serikali ina sehemu yake lakini huwezi kuendesha uchumi mkubwa kama huu kwa kupitia Serikali peke yake,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema “Lazima tukaribishe sekta binafsi katika kufanya kazi na sisi, sekta binafsi kuna kampuni nyingi, kuna watu mbalimbali ambao tungepena kushirikiana nao, lakini umhimu wa kuwashawishi diaspora ni suala nyeti kwetu sisi.”

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, amesema Serikali yake inafungua milango kwa diaspora katika utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Bluu, kwa kuwa wana uchungu na nchi yao.

“Tunaamini kwamba, mtu anapokuja kuwekeza akiwa na nasaba ya ile nchi anayoenda kuwekeza, atafanya vizuri zaidi sababu ile interest (maslahi) moyoni anakuwa nayo. Sababu ya leo kutaka kuzungumza nanyi, kuwashawishi kwamba milango iko wazi nyumbani, tunawakaribisha mrudi kufanya kazi na sisi,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amewaomba wawe mabalozi wazuri wa Zanzibar, katika nchi wanazoishi, ikiwemo kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza visiwani humo.

“Tungependa muweze kuzunguzma, muwe mabalozi wazuri kwa niaba ya nchi. Muwashawishi mnaowafahamu ambao wanaweza kuja kuwekeza, natambua huko nje kuna watu wengi wana utaalamu na ujuzi,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amewaita diaspora wanaotamani kurejea nyumbani, akiwaahidi kuwasaidia.

“Ningependa niwashawishi diaspora, kwa wale wanaopenda kuja kufanya kazi na sisi, kurudi nyumbani milango iko wazi. Tutawasilikiza, tutawasaidia, tutahakikisha tunatumia ujuzi wao kukuza uchumi wa Zanzibar,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema katika utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Bluu, Serikali yake imeweka vipaumbele kwenye sekta sita, ikiwemo bandari, uvuvi wa baharini, mafuta na gesi, pamoja na kilimo cha zao la mwani.

“Sehemu kubwa sana itatumika kama bandari, kwa hivyo ni eneo muhimu kwa visiwa na unapokuwa na visiwa, lazima suala la bandari lichukue kipaumbele. Sekta nyingine ni usafiri wa baharini kwa kuweka vyombo vya usafiri, sababu tunataka Zanzibar iwe kitovu cha usafirishaji bidhaa nje ya nchi,” amesema Rais Mwinyi na kuongeza:

“Sekta nyingine ni ya mafuta na gesi, tumegundua tuna mafuta na gesi asilia. Kwa maana hiyo tunakaribisha wawekezaji tuweze kuzalisha kwa wingi, kwani tukianza kufanya hivyo uchumi wa Zanzibar utapaa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *