RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli amesema, Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 utafanyika kwa amani, huru na haki huku akionya yeyote atakayethubutu kuuvuruga atachukuliwa hatua kali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne tarehe 16 Juni 2020 wakati akilivunja Bunge la 11 la Tanzania.
Kuvunjwa kwa Bunge hilo alilolizindua tarehe 20 Novemba 2015, kunatoa fursa ya kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi mkuu.
Rais Magufuli amesema, “tumejipanga kuhakikisha uchaguzi huu, unakuwa huru na haki.”
“Tutasimamia uchaguzi huru na haki kwa vyama vyote na hii ndiyo demokrasia ya kweli. Vyama vya siasa na wanasiasa kujiandaa vizuri katika uchaguzi huu,” amesema huku akishangiliwa na wabunge.
Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kuvisihi vyama vya siasa , “kutoa fursa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.”
Kiongozi huyo mkuu amewasihi wananchi kuepuka pepo la, “matusi na kejeri, matusi na kejeri hayajengi. Sisi sote ni wamoja, tukabishane kwa hoja na kushindanisha ilani yetu.”
Akihitimisha eneo hilo la uchaguzi, Rais Magufuli amesema, “kwa yoyote atakayetaka kuleta vurugu katika uchaguzi huu, namtahadharisha kwamba Serikali iko macho.”
Rais Magufuli amelivunja Bunge hilo hadi pale litakapoitishwa tena kwa mujibu wa sheria.
Usije ukawa kama ule uchaguzi wa mitaa kwa sababu katika folu waliandika St badala ya Street