Saturday , 27 April 2024
Home Kitengo Maisha Afya Puto lampunguza Msechu kilo 17, aongezewa maji
AfyaTangulizi

Puto lampunguza Msechu kilo 17, aongezewa maji

Spread the love

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili Mloganzila imesema hadi sasa imetoa huduma ya kupunguza uzito kwa watu 128 wenye uzito uliopitiliza kwa kutumia puto maalum (intragastic balloon), akiwamo Msanii na balozi wa puto hilo, Peter Msechu aliyepunguza kilo 17 kutoka kilo 144 alizokuwa nazo miezi sita iliyopita. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Huduma hiyo pamoja na kupunguza uzito imeelezwa kuwa na mafanikio ikiwemo kuwawezesha wateja hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi tofauti na ilivyokuwa awali.

Akizungumzia huduma hiyo jana Kaimu Mkuu wa Idara ya Upasuaji MNH-Mloganzila, Dk. Erick Muhumba amesema  kati ya watu hao 128 waliofanyiwa huduma hiyo wanawake wanne.

Amesema wanawake hao wamefanikiwa kupata ujauzito ambapo mmoja wao alikaa zaidi ya miaka sita bila kupata ujauzito kutokana na tatizo la uzito uliopitiliza.

Dk. Muhumba ameongeza kuwa zaidi ya watu 12 wameondolewa puto hilo kutokana na uzito wao kupungua na wachache wameondolewa kutokana na maudhi madogo madogo waliyoyapata kutokana na kuwekewa puto hilo hivyo kupelekea kuliondoa.

“Wapo baadhi ya wateja wetu takribani wanne tuliwawekea puto lakini tumelazimika kuliondoa kutokana na maudhi madogo madogo ikiwemo kutapika, lakini wengi wao huduma hii imekuwa rafiki na yenye mafanikio makubwa na wapo ambao wametoa baada ya uzito kupungua” amesema Dk. Muhumba

Dk. Muhumba amefafanua kuwa wapo ambao wameongeza maji au kupunguza maji kwenye puto kulingana na mahitaji ya wateja.

Ametoa mfano kuwa miongoni mwa waliongezewa maji kwenye puto kwa lengo la kuendelea kupunguza uzito ni msanii na balozi wa puto Mloganzila, Peter Msechu.

Akizungumzia hatua hiyo, Msechu amesema kwa kipindi cha miezi sita amepunguza takribani kilo 17 kutoka 144 alizokuwa nazo awali na ameona umuhimu wa kuongeza maji kwenye puto kutokana na kuwa na kasi ndogo ya uzito kupungua.

Msechu ameongeza kuwa tangu awekewe puto ameendelea kufanya majukumu yake kwa muda mrefu bila kuchoka.

Pia amebainisha kuwa uzito wake haujapungua kwa kasi kama alivyotarajia kutokana na kutofanya mazoezi kama alivyoshauriwa na wataalamu hali iliyotokana na ratiba yake kusongwa na majukumu mengi ya kitaifa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Afya

Mloganzila yajipanga kupandikizaji wa ini

Spread the love  HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imesema kutokana na uwekezaji uliofanywa...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!