December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Profesa Lipumba amkumbusha IGP Sirro saa yake

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

Spread the love

 

MWENYEKITI wa chama cha siasa cha upinzani nchini Tanzania- Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka InspektaJenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuendelea kutafakari na kuitafuta saa yake ya mkononi aliyonyang’anywa na askari wake, baada ya kupigwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tabora…(endelea)

Pia, amelilalamikia Jeshi hilo la polisi kwa kuvuruga shughuli za chama hicho zilizoandaliwa kufanyika hivi karibuni mkoani Tabora.

Akihutubia wananchi na wanachama wa chama hicho kwenye ukumbi mjini Tabora, hivi karibuni, Profesa Lipumba alidai Jeshi hilo limekuwa likiwavuruga katika shughuli zao na kwamba mkoani humo polisi waliandaa kuvuruga ili wasifanikishe malengo yao.

Alidai polisi walivuruga shughuli ya kuzindua mashina mawili ya kata za Mbugani na Mapambano na kuchangia damu kusifanyike katika ofisi zao, bali ukumbini, lakini hata hivyo walifanyia katika ofisi yao na kuchangia chupa 20 za damu kwa ajili ya jamii.

“Nitawasiliana na IGP, waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani, msajili wa vyama vya siasa na Rais, ili kutoa maelezo hayo na kutaka hatua zichukuliwe kuondosha tatizo hilo sugu la kuvuruga demokrasia ya siasa nchini, na kutafuta suluhisho la kudumu,” alisema Profesa Lipumba

Alisema atamshauri Rais Samia Suluhu Hassan atembee kwenye kauli zake za awali na kuzitekeleza kwa vitendo, kwa kuishi na kutetea demokrasia ya kweli, yenye msingi wa maendeleo na aisimamie, ili kulinda heshima yake na utu wa Watanzania.

IGP Simon Sirro

Mwenyekiti huyo alisisitiza, haki ikiwapo wananchi watanufaika, kwa kuwa watafanya mambo yao kwa uhuru na Rais atajiletea heshima na kukumbukwa na jamii, kwamba alisimamia na kutekeleza kauli zake kwa vitendo, na kwa uungwana na hivyo kazi ya kugombea tena itakuwa nyepesi kwake.

Aliwataka wana CUF kutokatishwa tamaa na ugumu uliopo, bali wajipange kupambana nao kwa kupigania haki ya kweli, wakisisitiza Tume huru ya uchaguzi ipatikane, ili uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia ufanyike.

“Jamani tujipange, tujenge mtandao imara, madhubuti na wa kisayansi wa chama, na tushikamane upya tukitambua kuwa ushindi wa CCM mwaka 2025, utatokana na Rais kutekeleza maazimio aliyojiwekea kwa haki na kweli mtupu, vinginevyo tunajipanga kuchukua nafasi na kutumia fursa,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Diwani wa Silambo-Ulyankulu, Wilaya Kaliua, Mashaka Muka (CUF), alidai kuwa kuna wananchi wake watano wanashikiliwa na Polisi tangu Oktoba mosi mwaka huu na hawajulikani waliko, ambapo alimwomba Mwenyekiti huyo alishughulikie ili kujua waliko wananchi hao.

Aidha, Mloke Jafari mwanachama wa CUF kata ya Kidongochekundu, alimwomba Mwenyekiti kueleza jitihada zake za kuleta maendeleo zilikokwamia na awape matumaini mapya wanachama ili kujengea imani mpya.

error: Content is protected !!