CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeahidi kumrudisha Profesa Mussa Assad, katika nafasi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kimeeleza kwamba, kitafanya hivyo endapo kitafanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020 na kuunda Serikali.
Ahadi hiyo imeanishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya uchaguzi huyo ya ACT-Wazalendo, iliyopitishwa jana tarehe 5 Agosti 2020, na Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ilani hiyo, ACT-Wazalendo itamrudisha kazini Prof. Assad ili amalize muda wake wa kazi kwa mujibu wa Katiba.
“Serikali ya ACT-Wazalendo itamrejesha kazini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Assad ili kumaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba,” inaeleza ahadi hiyo.
Tarehe 3 Novemba 2019 Rais Magufuli alimteua Charles Kichere kuwa CAG, baada ya Prof. Assad kufai kumaliza muda wake wa miaka 5, tarehe 4 Novemba 2019.
Hata hivyo, mwezi Januari mwaka huu Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo alifungua Kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga kuondolewa kwa Prof. Assad kwenye nafasi ya CAG, kwa madai kwamba hatua hiyo ilikuwa kinyume cha Katiba.

Katika Kesi hiyo ya Kikatiba Na.1/2020 iliyofunguliwa na Wakili Rugemeleza Nshala kwa niaba ya Zitto, mwanasiasa huyo anaiomba mahakama kutamka kwamba uteuzi wa CAG mpya ulikuwa kinyume na Katiba.
Kwa madai kwamba, Prof. Assad hakuwa ametimiza muda wa kustaafu (hakutimiza miaka 60 ya kustaafu).
Wakati huo huo, Ilani ya ACT-Wazalendo inaeleza, kwamba serikali ya chama hicho itaimarisha utendaji wa Ofisi ya CAG pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Ilani hiyo inaeleza kuwa, uteuzi wa viongozi wa taasisi hizo utaidhinishwa na Bunge baada ya uteuzi wa Rais.
“Serikali ya ACT-Wazalendo itaimarisha taasisi za kusimamia uwajibikaji kama Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT), Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kwa kuhakikisha mchakato wa uteuzi wa wakuu wa Taasisi hizo unaidhinishwa na Bunge baada ya uteuzi wa Rais,” inaeleza Ilani ya ACT-Wazalendo.
Leave a comment