May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi wataja chanzo mauaji Sinza

Spread the love

 

JESHI la Polisi  Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, limesema chanzo cha tukio la mauaji ya watu wawili katika Baa ya Lemax iliyoko Sinza mkoani humo, ni ulevi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi, tarehe 18 Julai 2021 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Ramadhan Kingai, akizungunza na MwanaHALISI Online kwa simu.

Tukio hilo lilitokea jioni ya jana tarehe 17 Julai 2021, katika baa hiyo baada ya Marehemu Alex Koroso, kumuuwa kwa kumpiga risasi Marehemu Gift Mushi, kisha kujiuwa mwenyewe kwa risasi.

Akizungunzia tukio hilo, Kamanda Kingai amesema  Alex alifanya tukio hilo, kutokana na kuzidiwa na ulevi.

Amesema kuwa, usiku wa kuamkia tukio, tarehe 16 Julai 2021,  Alex alikesha anakunywa bia katika Baa ya Element, kisha asubuhi yake alienda katika Baa ya Lemax, alikotekeleza mauaji hayo.

“Marehemu Alex alizidiwa na ulevi, kwani inasemekana amekesha akinywa katika baa ya Element. Asubuhi akaamkia Lemax ambapo amefanya mauaji na yeye kujiua. Ila ipo taarifa Alex tangu mwanzo silaha hii amekuwa akiitoa mara kwa mara mbele ya watu,” amesema Kamanda Kingai.

Kamanda huyo wa Polisi amesema, Alex alianza kutoa maneno machafu katika baa hiyo na kwamba, Gift alivyomshauri aache kufanya akaanza kurusha risasi hovyo na kumpiga bila kosa.

“Inasemekana hakukuwa na ugomvi ila ushauri wa Gift ndiyo ulipelekea kifo chake,  kwani Alex alianza kuwatukana wenzake kwa kuwaambia wanajifanya wao ni usalama na maneno mmengine makali,” amesema Kamanda Kingai.

Aidha, Kamanda Kingai amesema Polisi wanaendelea kuchunguza undani wa tukio hilo, ili kujua kama Alex alipewa  silaha hiyo lini na sababu za kuimiliki.

Kamanda Kingai ametoa wito kwa wananchi wanaomiliki silaha, kutozitumia vibaya kwa kuwadhuru wenzao.

“Nitoe raia kwa wananchi wakipata silaha waache ushamba, watambue kuwa wamepewa silaha hizo ili ziweze kuwalinda wao na sio kuuwa watu,” amesema Kamanda Kingai.

error: Content is protected !!