Friday , 26 April 2024
Home Kitengo Biashara NMB yazindua teleza kidigitali, Majaliwa awapa heko
Biashara

NMB yazindua teleza kidigitali, Majaliwa awapa heko

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede (kulia), baada ya kuzindua huduma mpya za fedha ambazo zitatolewa kidigitali na Benki ya NMB “Teleza Kidigitali” katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma, Aprili 11, 2022. Kutoka kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hassan Hamad Chande.
Spread the love

BENKI ya NMB nchini Tanzania, imefanya mapinduzi makubwa ya kibenki kwa kuzindua huduma kubwa tatu kupitia kampeni yake ya ‘Teleza Kidigitali.’ Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Huduma hizo zinamwezesha mteja wa benki hiyo kupata mkopo kupitia simu ya mkononi bila kufika kwenye ofisi yoyote ya NMB bila dhamana.

Huduma hizo zimezinduliwa leo Jumatatu, tarehe 11 Aprili 2022 na jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Pia, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof Florens Luoga amehudhuria.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna, akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma mpya za fedha ambazo zitatolewa kidigitali na Benki ya NMB “Teleza Kidigitali” katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma, Aprili 11, 2022.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao ni wa kwanza kufanywa na sekta ya Benki nchini, Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema huduma hizo zitaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kibenki nchini.

Ameitaja huduma ya kwanza ni mikopo kwa njia ya kidijitali ambayo NMB wameiita huduma ya MshikoFasta.

“Huduma hii ya mikopo kidijitali itamuwezesha mteja wa Benki ya NMB kujipatia mkopo kwa uharaka na kwa urahisi kabisa kupitia simu yake ya mkononi bila kufika kwenye tawi lolote la Benki ya NMB na bila kuweka dhamana,” amesema Ruth.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma mpya za fedha ambazo zitatolewa kidigitali na Benki ya NMB “Teleza Kidigitali” katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma, Aprili 11, 2022.

“Huduma hii itapatikana kupitia NMB mkononi kwa simu za aina zote, simu janja (kwa App) ama kwa kutumia simu za kawaida (kwa kutumia USSD). Mteja wa Benki ya NMB, kwa kutumia huduma hii ataweza kukopa mpaka Sh.500,000 ndani ya muda mfupi, kupitia simu yake ya mkononi,” amesema

Afisa mtendaji mkuu huyo amesema, “haya ni mapinduzi makubwa kwenye sekta ya kibenki Tanzania na inaendelea tu kuthibitisha dhamira yetu ya kuendelea kuwa kinara katika mapinduzi ya huduma bora za kibenki na za kibunifu hapa nchini.”

Amesema imezoeleka sehemu nyingi mabenki kutoa huduma zinazofanana na hii, kupitia mitandao ya simu, lakini kwa ubunifu waliokuja nao, wateja wa NMB watakopeshwa moja kwa moja na benki na mikopo hii inaweza kurejeshwa ndani ya siku 1, siku 7, 14, 21 au siku 28.

Amesema riba ya mikopo hii itategemea kiwango kilichokopwa pamoja na muda utakaotumika kurejesha mkopo na mteja anapochukua mkopo, mtandao utaonyesha atarejesha Shilingi ngapi kwa muda aliouchagua.

Ruth amesema, lengo la NMB ni kuhakikisha urahisi na uharaka wa kupata mikopo hususani kwa makundi ya wajasiriamali wadogo na wa kati, kama mama Ntilie, Bodaboda, machinga ambao wengi hawako kwenye mfumo rasmi kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi, kwa sababu ya aina za biashara zao, au kwa kukosa dhamana kwa ajili ya mikopo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, wiki iliyopita tulitembelea soko la wamachinga na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na tulijadili kwa kirefu maono makubwa aliyonayo Mkuu wa Mkoa kwa Wamachinga na wafanyabiashara wadogo, na ni furaha kwetu kuona kwamba kwa kutumia NMB MshikoFasta tunakwenda kupunguza changamoto ya ugumu wa kupata mikopo na kuweza kusaidia kuongeza mitaji kwa makundi haya,” amesema

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akibonyeza kitufe, kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa huduma mpya za fedha ambazo zitatolewa kidigitali na Benki ya NMB “Teleza Kidigitali” katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma, Aprili 11, 2022. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hassan Hamad Chande, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna.

Amesema kila kukicha shughuli za kibenki zinabadilika, na teknolojia imekuwa ndio chanzo kikubwa cha mabadiliko haya, hususani jinsi mabenki yanavyoweza kutoa huduma mbalimbali, kidigitali.

“Sisi Benki ya NMB hatujabaki nyuma, tunaendelea kutumia rasilimali tulizonazo kuwekeza kwenye tekinolojia ili kuendelea kuleta masuluhisho kwenye jamii, kuendelea kuchagiza ukuaji wa teknolojia kwenye nchi yetu, na hivyo basi kuchangia katika ukuaji wa uchumi,” amesema

Mtendaji huyo mkuu wa NMB, ametaja huduma ya pili iliyozinduliwani NMB Pesa Wakala ambayo ni maboresho ya huduma ya NMB Wakala iliyopo sasa.

Amesema NMB Pesa Wakala, ni wakala atakayetumia simu yake ya mkononi kuwa Wakala wa Benki ya NMB na kuwezesha wateja wake kuweka na kutoa pesa kupitia simu zao za mkononi kama walivyo mawakala wa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu.

“Kwa taarifa tu Mheshimiwa Waziri Mkuu, Benki ya NMB tayari ina Mawakala zaidi ya 11,000. Kupitia huduma ya NMB Pesa Wakala, tunalenga kufikia idadi ya mawakala 100,000 nchi nzima ndani ya miaka mitano ijayo,” amesema.

“Kikubwa zaidi, NMB Pesa Wakala sio tu itaenda kurahisisha huduma kwa wateja wa NMB, lakini pia ni sehemu ya kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania wenzetu. Ili kuwa Wakala wa NMB Pesa, sasa utahitaji tu simu yako ya mkononi, (simu janja (smart phones) au za kawaida maarufu kama ‘kitochi’), leseni ya biashara na kitambulisho cha Taifa,” amesema Ruth.

Huduma ya tatu ni huduma ya Lipa Mkononi ambayo ni huduma ya malipo kwa njia ya QR code au Lipa namba.

Amesema huduma hii inawawezesha wafanyabiashara wakubwa na wadogo nchini kupokea malipo kwa njia za kidijitali ambapo linaruhusu kupokea malipo kirahisi, haraka na kwa usalama zaidi kutoka makampuni yote ya simu na mabenki ambayo yameunganishwa na mtandano wa Mastercard au VISA.

Amesema huduma hii itasaidia utunzaji fedha kwa wafanyabishara,na itaongeza usalama wa fedha zao maana hakuna haja ya kukaa na pesa taslimu au kupata usumbufu wa kutafuta chenji.

Alimhakikishia Waziri Mkuu kuwa NMBitaendelea kuja na masuluhisho bora na nafuu kwa watanzania na uwajibikaji wao kwa jamii utabaki kuwa katika viwango vya juu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Dk. Edwin Mhende, amesema lengo benki hiyo ni kuboresha na kurahisisha huduma zao na kuzifanya kuwa za kidigitali zaidi huku wakienda sambamba na maendeleo ya kiteknolojia ulimwenguni na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa NMB (2020-2025).

Amesema NMB wanatambua umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya tehama kuwafikia na kuwajumuisha Watanzania wengi kwenye mfumo rasimi wa kifedha kwa maendeleo ya wananchi.

“Na sisi NMB, kwa kutumia vijana wetu makini ambao ndio chachu ya ubunifu huu tunaouzindua leo, tunajitahidi kukimbia mwendo sawa na maendeleo hayo katika Taifa letu na katika nchi za Bara la Afrika zilizopo ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA),” amesema na kuongeza:

“Ni kwa msingi huo, leo hii NMB tunakuja na “TELEZA KIDIGITALI”, kampeni inayolenga kutoa elimu mahususi kuhusu mojawapo ya suluhishi mpya za kidigitali kutoka Benki ya NMB zinazo rahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza ulazima wa wateja wetu kufika kwenye matawi kupata huduma.”

Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Luoga, ameipongeza NMB kwa kwenda na kasi ya maendeleo ya kidigitali na hasa kutumia vijana wao wa ndani kuanzisha huduma hizo.

Amesema uzinduzi wa huduma hizo kidigitali ni muhimu kwa jamii lakini pia inaonesha ushindani wa kibenki uliopo nchini.

Akizindua huduma hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema tukio lililofanywa na NMB kuzindua huduma hizo, inaonesha kuwa benki hiyo ni kiboko.

“Yaani mtu anataka mkopo wa Sh.300,000, au Sh.500,000, haindi kwenye tawi lolote la benki, haonani na mtumishi yoyote wa Benki, atabaki kwenye simu yake, anaomba mkopo na anaupata, hayo ni mageuzi makubwa sana katika sekya ya kibenki,” amesema

Majaliwa amesema, NMB kwa huduma hizo inakwenda kuchochea maendeleo kwani wananchi wengi wataweza kupata mitaji ya mkopo wa riba nafuu na hivyo kuepukana na wajanja wanaotoa mikopo kwa riba kubwa.

Majaliwa ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi za fedha kubuni mikakati na mbinu zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata huduma rasmi za kibenki kwa gharama nafuu ili waweze kujiongezea kipato na kujikwamua na umasikini.

Amesema taasisi hizo hazina budi kuiunga mkono Serikali kwa kubuni mikakati mbalimbali ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kukuza uchumi sambamba na kubuni masuluhisho rahisi kwa watumiaji wa kawaida.

Amesema benki nchini hazina budi kubuni zaidi namna ya kutafuta masuluhusho yaliyo katika sekta za kifedha. “Hongereni NMB kwa ubunifu huu ambao utavutia makundi yote ya kijamii, huduma hii itawezesha wateja wenu kupata huduma ya mikopo kiganjani.”

Majaliwa amesema amevutiwa na huduma hizo ikiwemo ya MshikoFasta ambayo inakwenda kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa haraka kwa mama lishe na baba lishe, bodaboda, wafanya biashara wadogo na wananchi wote wa kawaida.

“Ninaipongeza NMB kwa kuja na suluhisho hili, naamini asilimia kubwa ya Watanzania watanufaika sana na huduma hii katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na changamoto ya ajira kwa vijana. Hii ni fursa ya vijana kujipatia mitaji,” amesema.

Amesema huduma hiyo ya mikopo ya kidigitali inakwenda kumaliza kabisa tatizo la ugumu wa kupata mikopo. “Hii ni hatua kubwa sana kwenye sekta ya kibenki Tanzania. Tukio hili linapeleka ujumbe kwa Watanzania wa kuwataka wasihangaike kupata mikopo ya kuanzisha biashara zao kwa kuwa fedha ipo NMB.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo katika hatua za awali za maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali pamoja na Mkakati wa Taifa wa Brodibandi utakaowezesha asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za intaneti yenye kasi ifikapo 2025.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Biashara

Orb of Destiny kutoka Meridianbet kasino ushindi kwa njia 14  

Spread the love  ORB of Destiny ni mchezo wa sloti kutoka kwa...

Biashara

Jiandalie Strawberry Cocktail yako nyumbani huku unacheza kasino 

Spread the love  UTAANDAA matunda yako unayotaka kutumia unaweza kutumia Strawberry, Cantaloupe...

Biashara

420 Blaze It chimbo jipya la kuchota mihela Meridianbet kasino 

Spread the love  JE, umewahi kucheza mchezo wa droo wenye droo 10?...

Biashara

Exim yawainua kiuchumi wanawake wajasiriamali kupitia mpango wa WEP

Spread the love  BENKI ya Exim kupitia Mpango wake wa Kuwawezesha Kiuchumi...

error: Content is protected !!