Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko NMB yazindua tawi la 229 Arusha, BoT yatoa neno
Habari Mchanganyiko

NMB yazindua tawi la 229 Arusha, BoT yatoa neno

Spread the love

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeipongeza Benki ya NMB kwa kuwa kinara miongoni mwa mabenki 44 nchini kwa ubunifu wa kuchagiza ukuaji wa sekta ya fedha kwa kutanua mtandao wa matawi na kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki, hivyo kukuza kiwango cha amana za wateja. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa BoT, Kanda ya Arusha, Ibrahim Malogoi, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB Kwa Mrombo jijini Arusha.

Tawi hilo linakuwa tawi la 229 kwa Benki hiyo nchini, hafla iliyohudhuriwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi.

Uzinduzi wa Tawi la Kwa Mrombo linalokuwa la sita la Benki ya NMB jijini Arusha, huku likiwa ni la 12 kwa mkoa huo na la 43 Kanda ya Kaskazini, umefanyika Jumatano Mei 3, 2023 sambamba na makabidhiano ya msaada wa madawati 100 kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kwa ajili ya Shule ya Msingi Msasani iliyopo jirani na tawi hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella (Katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi jipya la Kwa Mrombo la Benki ya NMB katika hafla maalum ya uzinduzi wa Tawi hilo mkoani hapo. Tawi hilo linakuwa Tawi la 6 la Benki ya NMB kwa jiji la Arusha, na la 229 kwa nchi nzima. Wapili kushoto ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, wapili kulia ni Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Arusha, Ibrahim Malogoi, kulia ni Naibu meya wa jiji la Arusha, Veronica Hosea na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Mtandao wa matawi wa Benki ya NMB, Donatus Richard.

 Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Malogoi alisema sekta ya fedha inakua kwa kasi kubwa nchini na kwamba wao kama ndio wasimamizi wakuu wa sekta hiyo Tanzania, wanafarijika kwa ongezeko la matawi ya benki nchini, huku akipongeza uamuzi wa NMB kufungua tawi Kwa Mrombo, eneo ambalo linakua kwa haraka na kuongezeka kwa uhitaji wa huduma za kibenki. 

“Sekta ya Fedha inakua kwa kasi bila kupingwa, Tanzania tunazo benki 44, kati ya hizo Kanda ya Kaskazini zipo 28, huku mkoa wa Arusha pekee zikiwepo 26 zinazotoa huduma. Tawi hili ambalo limekuja kwa wakati sahihi, ni ushahidi wa kukua kwa sekta hii, kwani linakuwa ni tawi la 988 ya matawi ya mabenki yote nchini.

“Kati ya matawi hayo, 196 yapo katika Kanda ya Kaskazini (Arusha, Tanga, Manyara na Kilimanjaro), huku tawi hili la NMB Kwa Mrombo likiwa la 65 mkoani Arusha. Sisi BoT tunafarijika kwa ongezeko hilo ambalo litaongeza kiwango cha amana kwa Mkoa na Kanda yetu, lakini pia kwa Taifa.

“Kwa rekodi zilizopo, hadi Desemba 2022, kiwango cha amana za wateja ni Sh. Trilioni 3.3, kati ya hizo Trilioni 1.4 ni amana za wateja waliopo mkoani Arusha pekee, ndio maana tunaamini kwa ujio wa tawi hili, NMB itaharakisha kukua kwa amana hizo,” alifafanua Malogoi. 

Kwa upande wake,  RC Mongella alisema anaamini NMB Tawi la Kwa Mrombo ni kichocheo cha ukuaji kiuchumi kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi wa Arusha, na kuwa uwingi wa matawi mkoani mwake, pamoja na uwekezaji mkubwa kidijitali uliofanywa na NMB, utaondoa foleni matawini zinazokwaza ustawi kiuchumi, hivyo kurahisisha mzunguko wa utafutaji na kuchochea fursa za maendeleo.

“Tawi hili, sambamba na mengineyo mkoani Arusha, linaenda kuwa kichocheo cha ukuaji wa haraka kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, mkoa na Taifa kwa ujumla, hasa ukizingatia uwekezaji mkubwa wa kidijitali uliofanywa na benki hii, ambao utachagiza upatikanaji wa huduma kirahisi matawini na kwa njia za mtandao na hivyo kumaliza kero ya safari ndefu za kufuata huduma za kibenki. 

 “Wito wangu kwa wana Arusha ni kutumia vema fursa za kustawi kiuchumi zinazoletwa na NMB, ambayo ni Benki Salama inayozidi kuwa karibu na kila mtu. Wenye akaunti waendelee kunufaika na huduma, na wasio nazo wakati wao wa kufungua ni sasa, ili kila mmoja awe sehemu ya kukuza pato lake binafsi na kuongeza faida ya benki, ambayo imekuwa na matumizi sahihi ya fungu la Uwajibikaji kwa Jamii kama tulivyoona ikitoa misaada mashuleni, hospitalini na zahanati.

 Awali, Mponzi alimshukuru RC Mongella kwa kutenga muda wa kushiriki uzinduzi wa tawi hilo ambalo linaenda kuwa chachu ya maendeleo na mkombozi wa wateja wao, wakiwemo mawakala wa NMB waliotapakaa katika mji wa Arusha na mikoa mikoa jirani ya Kanda ya Kaskazini.

 “Licha ya ukweli kwamba tawi hili litakuwa kichocheo cha ukuaji wa haraka kiuchumi, pia litarahisisha upatikanaji huduma kwa wateja wetu, hususani mawakala wa NMB waliotapakaa hapa Arusha na mikoa ya jirani.

 “Tunajivunia kukua kwa mtandao wetu wa matawi, sambamba na uwekezaji mkubwa kidijitali, ambao unampa fursa mteja kufungua akaunti kwa simu na hata kupata huduma, zikiwemo za Mikopo midogo isiyo na dhamana ya Mshiko Fasta,” alibainisha Mponzi mbele ya Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Dismas Prosper.

 Mponzi aliushukuru Serikali kwa kuboresha mazingira ya taasisi za fedha kutoa huduma kwa ufanisi, na kwamba wanajivunia hilo wakati huu wakati huu ambao benki yake inaadhimisha Mtaka 25, sherehe zinazoenda sambamba na kampeni endelevu ya upandaji miti milioni moja kwa mwaka huu, iliyozinduliwa Machi mwaka huu mjini Dodoma na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!