Saturday , 27 April 2024
Home Kitengo Biashara NMB yaweka historia mpya, faida yapaa hadi bil. 775
BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yaweka historia mpya, faida yapaa hadi bil. 775

Spread the love

BENKI ya NMB imeweka rekodi mpya ya ufanisi kiutendaji kwa kutengeza faida kabla ya kodi ya TZS bilioni 775 na kupata mafanikio mengine kifedha ambayo imesema yamechangia kubadilisha maisha ya watu na kuwa na tija katika uchumi wa taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwananchi

Akitangaza matokeo ya mafanikio hayo ya kihistoria leo Jumanne jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Ruth Zaipuna aliwaambia waandishi wa habari kuwa rekodi mpya ya faida imetokana na ukuaji mkubwa wa mikopo, kuongezeka kwa wateja na miamala pamoja na amana, ubora wa mikopo na kiwango cha juu cha ufanisi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wapili kushoto) akipokea taarifa ya fedha ya Mwaka ya Benki ya NMB kutoka kwa Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki hiyo, Juma Kimori (wapili kulia) katika hafla maalum ya kutoa taarifa hiyo ya fedha kwa wanahabari Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mkuu wa wateja wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao na Kushoto ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi.

Kiongozi huyo alibainisha kuwa faida hiyo kubwa imepatikana baada ya jumla ya mapato ya mwaka 2023 kufikia Sh 1.4 trilioni kutokana na ukuaji wa asilimia 24 wa mapato ya riba na asilimia 15 ya mapato yasiyotokana na riba.

“Kutokana na ufanisi huu, faida kabla ya kodi imeongezeka kwa asilimia 26 hadi Sh 775 bilioni huku faida baada ya kodi ikifika Sh 542 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 kwa mwaka. Hiki ni kiwango kikubwa cha faida na cha kihistoria kwa benki ya NMB na sekta nzima ya fedha nchini,” Zaipuna amesema.

Katika kuonyesha ukubwa wa ukuaji huo, kiongozi huyo alibainisha kuwa mwaka 2020 wakati NMB inaweka Mpango Mkakati wa Muda wa Kati (2021-2025), jumla ya mapato zilikuwa ni Sh 842 bilioni pekee, huku faida kabla ya kodi na baada ya kodi zikiwa Sh 296 bilioni na Sh 206 bilioni mtawalia.

“Mizania ya Benki imeendelea kukua na kufikia jumla ya mali ya Sh 12.2 trilioni ikiwa ni ukuaji wa asilimia 19 kwa mwaka, huku ukwasi na mtaji wa Benki ukiwa imara na juu ya viwango vya Benki kuu. Ukuaji huu ulitokana hasa na kukua kwa amana za wateja kwa asilimia 12, pamoja na ongezeko la mikopo la asilimia 28,” ameongeza.

Aidha, ufanisi mkubwa kwenye gharama za uendeshaji na ubora wa mikopo ulitokana na kuboreshwa zaidi kwa uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato kufikia hadi asilimia 39, wakati uwiano wa mikopo chechefu ulishuka hadi asilimia 3.2, viwango ambavyo ni chini ya ukomo wa kikanuni wa Benki Kuu wa asilimia 55 na asilimia tano mtawalia.

“Tunajivunia ufanisi mkubwa na matokeo chanya ya kiutendaji yaliyopatikana katika maeneo muhimu ya utekelezaji wa mkakati wetu, ikiwemo ujumuishwaji wa watanzania kwenye sekta rasmi ya kifedha, utoaji wa huduma bora kwa wateja, na uwekezaji wa kimkakati kwa wafanyakazi wetu, utawala bora na uwekezaji kwenye teknolojia ili kuongeza thamani,” Zaipuna amebainisha.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa ufanisi na matokeo haya ya kiutendaji yamekuwa pia na matokeo chanya hata kwenye bei ya hisa za NMB iliongezeka kwa asilimia 49 kutoka Sh 3,020 hadi kufikia Sh 4,500 kati ya Januari na Disemba 2023.

Aidha, ongezeko hili la bei ya hisa limefanya mtaji wa Benki ya NMB kwenye soko la hisa kufikia Sh 2.25 trilioni kutoka Sh 15. trilioni za Disemba 2022.

Hili limepelekea NMB kuwa benki kubwa zaidi iliyoorodheshwa kwenye soko la hisa Tanzania na masoko yote ya hisa Afrika Mashariki kwa kigezo cha thamani ya kampuni kwenye soko la hisa yaani market capitalization.

Pia NMB sasa ni kampuni ya nne kwa ukubwa kwa kampuni zilizoorodheshwa Afrika Mashariki, baada ya Safaricom ya Kenya, Tanzania Breweries, na MTN-Uganda na ni ya 26 kwa ukubwa kati ya kampuni zilizoorodheshwa Kusini mwa Jangwa la Sahara (ukiondoa Afrika Kusini).

Hii ni mara ya kwanza kwa NMB kuwa katika orodha hiyo, na kuwa benki pekee ya Tanzania kuwahi kuingia kwenye orodha ya kampuni 30 kubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Mafanikio yaliyopatikana mwaka 2023 yanaonyesha jukumu la NMB kuendelea kuwa injini ya ustawi wa kiuchumi nchini, na mwezeshaji wa kuzifungua fursa mpya kwa wateja na wadau wetu wote Tanzania,” Zaipuna amefafanua.

Amesema kwa mwaka 2024, NMB itaendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki nchini hasa vijijini na maeneo yaliyo pembezoni na hivyo kuongeza ujumuishwaji wa watanzania wengi kwenye sekta rasmi ya kibenki kupita suluhisho bunifu kama NMB Pesa.

Naye Afisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Juma Kimori, amesema ufanisi wa mwaka jana ni ishara ya nidhamu na umakini katika kutekeleza kwao Mpango Mkakati wa Muda wa Kati ambao moja ya malengo yake ni kuhakikisha NMB inaendelea kuwa mbia nambari moja wa Serikali na jamii nzima ya Watanzania katika kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Rais Samia kuzindua gazeti litakalotoa habari za wafanyakazi Tanzania

Spread the loveSHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), liko mbioni kufufua...

Habari Mchanganyiko

GGML yaja na teknolojia za kisasa maonesho ya OSHA Arusha

Spread the loveKATIKA kuelimisha wananchi na washiriki wa maonesho ya usalama na...

Biashara

Orb of Destiny kutoka Meridianbet kasino ushindi kwa njia 14  

Spread the love  ORB of Destiny ni mchezo wa sloti kutoka kwa...

Habari Mchanganyiko

GGML, OSHA wawanoa mama lishe 50 kukabiliana na majanga ya moto

Spread the loveKampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na...

error: Content is protected !!