BENKI ya NMB Kanda ya Kaskazini nchini Tanzania imekabidhi msaada wa bati 200 kwa Shule ya Sekondari Olongadida, kata ya Qash na kompyuta 25 kwa shule saba zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara ili kusaidia kuboresha utoaji wa elimu kwa wanafunzi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Msaada huo imekabidhiwa na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Dismas Prosper kwa mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange.
Prosper alisema lengo la kutoa msaada huo ni baada ya kuona vikwazo vinavyowakabili wanafunzi katika wilaya ya Babati ambao walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda shule lakini kwa ukosefu wa kompyuta zinazosaidia katika utoaji wa elimu ya kidigitali.
Alisema, “wanafunzi wa maeneo haya wanasafiri umbali mrefu sana kwenda shule sababu ujenzi wa shule ya karibu haujakamilika, hivyo tumeleta mabati haya ili kukamilisha ujenzi wa shule hizi na kuwapunguzia wanafunzi wetu umbali wa kutembea kwenda shuleni.”
“Dunia ya sasa ni ya kiteknolojia zaidi na ndio maana tukaona tukubaliane na maombi ya shule za wilaya ya Babati kupata kompyuta ili kurahisisha ufundishaji wa somo hilo na kupunguza uhaba wa vifaa hivi katika shule zetu,” Alisema
Aidha Meneja huyo alisema lengo la kutoa msaada huo ni kwa ajili ya kusaidiana na serikali katika kutatua changamoto za wananchi hasa katika sekta ya elimu na afya huku akisema NMB kwa mwaka huu wametenga Sh.2 bilioni ili kuboresha huduma hizo kwa nchi nzima.
Naye mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange akipokea msaada huo katika Kijiji cha Olongadida, aliipongeza NMB kwa kuwa mshirika mwema wa maendeleo ya wilaya ya Babati.
Alisema serikali itaendelea kuzungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya kuendelea kutoa misaada kwa shule za wilaya hiyo.
Aidha, Twange aliwapongeza wananchi wa Kijiji hicho kwa kuchanga Sh.20 milioni pamoja na kutumia nguvu zao binafsi kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Olongadida.
Mkazi wa Kijiji cha Olongadida Hamis Rajab aliishukru NMB kwa kutoa msaada huo na kudai utasaidia kukamilisha haraka ujenzi wa shule hiyo na ili kusaidia wanafunzi waache kutembea umbali wa kilometa nane.
Akizungumza baada ya kupokea misaada hiyo, Mbunge wa Babati ambaye pia ni naibu waziri wa utamaduni, sanaa na michezo, Pauline Gekul aliwataka walimu wakuu kuzitunza vizuri kompyuta hizo ili zikasaidie idadi kubwa ya wanafunzi wanaopita katika shule hizo.
Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Anna Fissoo aliwapongeza NMB kwa msaada huo na kuahidi kutunza vifaa hivyo.
Leave a comment