May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Mkumbo ataka maafisa elimu kata wang’olewe kufidia pengo la walimu

Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo,

Spread the love

 

MBUNGE wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, ameishauri Serikali ifute kada ya maafisa elimu kata, ili kuziba changamoto ya upungufu wa walimu shuleni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mbunge huyo wa Ubungo, ametoa ushauri huo leo Jumanne, tarehe 10 Mei 2022, bungeni jijini Dodoma, akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.

“Tupunguze nafasi ya utawala katika elimu, tufute kada ya maafisa elimu kata ili tuimarishe menejimenti ya shule ili watu hawa waende kufundisha. Tunazungumza kupata walimu 36,000, hakuna sababu ya kuwa na maafisa elimu kata kama kuna uongozi mzuri,” amesema Prof. Mkumbo.

Aidha, Prof. Mkumbo ameishauri Serikali iweke malengo ya kuajiri walimu 20,000 hadi 30,000 kwa mwaka, ili kuziba pengo la idadi ya walimu, huku akishauri muda wa mafunzo ya ualimu uongezwe ili wanafunzi wakafundishe kwa vitendo shuleni kwa muda wa mwaka mmoja.

“Muda wa mafunzo ya ualimu katika vyuo vikuu uongezwe, uwe miaka minne na ule mwaka wa nne wote watumike kwenye mafunzo shuleni. Kwa hiyo tutapata walimu kati ya 15,000 mpaka 20,000 kila mwaka kutoka vyuo vikuu na hawa hatuwalipi waendelee kulipwa na bodi,” amesema Prof. Mkumbo.

Katika hatua nyingine, Prof. Mkumbo ameishauri Serikali irudishe utaratibu wa kutoa posho kwa walimu, ili kuwaongezea motisha ya kufanya kazi.

“Suala la motisha kwa walimu, naomba turudishe posho ya kufundisha kwa walimu na hapa tunazungumzia kitu kidogo, Sh. 4,000 kwa siku kwa walimu. Maana yake kwa siku tano analipwa Sh. 20,000 kwa mwezi ni Sh. 100,000, hii itahamasisha walimu na imekuwa muhimu sana na waliomba muda mwingi,” amesema Prof. Mkumbo.

error: Content is protected !!