VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliopo madarakani wametakiwa kuruhusu watia nia wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho kuchukua fomu hata katika nafasi watakazozitetea na kwamba kufanya hivyo watakuwa wametenda haki. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Hayo yalielezwa na diwani wa Kata ya Chanika Wilaya ya Ilala, mkoa wa Dar es salaam, Masaburi Ojambi, wakati akifungua semina kwa makada wa CCM ngazi ya matawi na Kata iliyofanyika leo Jumanne tarehe 9 Mei 2022 kwenye Kata hiyo.
Ojambi alieleza kuwa makatibu waache kasumba ya kuficha fomu kwa nafasi ambazo wanatarajia kuzitetea katika chaguzi unaoendelea hivisasa ndani ya chama hicho na badala yake watoe fursa kwa kila mhitaji ili demokrasi ichukuwe sehemu yake.
Mtoa mada katika semina hiyo, Mwinyimkuu Sangala aliwataka viongozi kufuata maadili na kanuni za chama kwa kupitisha wagombea wenye sifa na hivyo watakuwa wametenda haki na kupunguza malalamiko kwa watu wengine.
Hata hivyo aliwataka vijana kukimbilia kwenye vyuo vya ufundi stadi watakakoenda kupata ujuzi wa fani mbalimbali kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kila siku huku wakiongeza pato la taifa kwa kuwa watakuwa wanalipa kodi na ushuru kutokana na kazi watakazozifanya.
Naye mwenyekiti wa taasisi ya Elimu ya Furahika, Mohamed Ngwenje alitumia nafasi hiyo kutangaza ofa kwa vijana 250 ambao alidai watasoma bure kwenye chuo cha ufundi kinachoendeshwa na taasisi hiyo lengo ni kuwaandaa katika maisha ya kujitegemea.
Ngwenje alieleza fursa hiyo kwamba inatolewa kwa kila mwaka na kwamba kinachotakiwa kwa wazazi ni kuwanunulia watoto wao vifaa vya kazi watakayojifunza kwa kipindi hicho huku gharama za chuo zikilipwa na taasisi hiyo ya Elimu ya Furahika.
Aidha katibu wa mbunge wa jimbo la Ukonga, Jemes Uliuma alitoa pole kwa wakazi wa Kata ya Chanika na Zingi waliopatwa na janga la panya road huku akieleza azma ya mbunge kuzitembelea kwa ajili ya kujua changamoto walizonazo.
Uliuma alisema wananchi wa Kata hizo walivamiwa na vijana wa panya road na kushambuliwa kwa mapanga na marungu kitendo ambacho licha ya mbunge huyo kulaani lakini pia kimemfanya kuandaa ziara ya kwenda kwenye maeneo hayo.
Leave a comment