Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko NMB yafuturisha Dar, Majaliwa azitaka Serikali za Mitaa, Taasisi zijifunze kwao
Habari Mchanganyiko

NMB yafuturisha Dar, Majaliwa azitaka Serikali za Mitaa, Taasisi zijifunze kwao

Spread the love

BENKI ya NMB imewafuturisha wateja wake walio kwenye Mfungo wa Mwezi Ramadhani jijini Dar es Salaam, pamoja na kutoa misaada kwa vituo vya watoto waishio katika mazingira magumu, huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiziagiza Serikali za Mitaa na Taasisi za Fedha, zijifunze kwa NMB namna ya kuwathamini wenye uhitaji. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Hafla hiyo ya Iftar imefanyika jana Jumanne jijini Dar es Salaam, ikiwa ni ya tatu kuandaliwa na Benki ya NMB tangu kuanza kwa ibada ya Funga ya Ramadhani ambayo ni Nguzo ya Pili kati ya tano za Dini ya Kiislamu, ikitanguliwa na hafla zilizofanyika katika Visiwa vya Unguja na Pemba, ambako pia kulitolewa misaada ya kijamii kwa watoto wenye uhitaji.

Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na zaidi ya watu 1,200 wakiwemo wateja wa NMB, wadau, viongozi wa Serikali, Watoto wanaoishi Kwenye Mazingira Magumu wa Vituo vya Al-zam (cha Mbagala), Umrah (Magomeni Mikumi) na Tanzania Kwanza (Tuangoma, Kigamboni).

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kulia), akiagana na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Juma Kimori, baada ya kumalizika kwa hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhede.

Akizungumza mbele ya waalikwa hao, Waziri Mkuu Majaliwa alisema NMB inastahili pongezi kwa namna inavyoyajali makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo kusapoti jitihada za elimu katika sekta za elimu, afya, maji, michezo na elimu za fedha kwa wajasiriamali.

“Leo hii nitapokea kutoka kwa NMB zawadi maalum kwa ajili ya Watoto wenye uhitaji wa vituo vya Al-zam, Umrah na Tanzania Kwanza vya Dar es Salaam. Kwa hili NMB mmefanya jambo kubwa sana, mnataka watoto hawa wajione kuwa wana thamani sawa na wengine.

“Natambua kuwa licha ya kuwakumbuka watoto wenye uhitaji, mmekuwa pia mkichangia mahitaji kwenye shule zinazotumiwa na watoto wenye mahitaji maalum.

“Pia, NMB ni benki inayoongoza kwa hutoaji huduma hapa nchini kwa sasa, ambayo imetenga kiasi cha Sh. Trilioni 1 kwa ajili ya kuhudumia sekta ya kilimo nchini, hii ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anakamilisha miaka mitatu ya uongozi wake madarakani,” alisema.

Waziri Mkuu akaenda mbali zaidi kwa kusema NMB ambayo ni benki ya ubia, na Serikali ikiwa na hisa, ambapo imekuwa mnufaika wa hisa ilizonazo, akitolea mfano wa magawio makubwa, rekodi ikiwekwa mwaka 2023 ilikotoa gawio la Sh. Bilioni 45.3 kwa Serikali, kiasi  ambacho hakijawahi kutolewa na mbia yeyote wa Serikali kama gawio.

Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza watu wenye vituo vya Watoto Yatima na Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kimaendeleo katika umri wao, na kwamba NMB inaongoza njia inayopaswa kupitwa na taasisi nyingine kiasi cha kutaka ziige mwenendo huo.

“Kama ambavyo nimetoa wito kwa taasisi na wadau wengine kuiga kwa NMB, Nitumie fursa hii pia kuziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa – ambazo ni Taasisi ya Serikali, Wastahiki Mameya mpo hapa, wakuu wa Wilaya mpo hapa, Madiwani wachache wawakilishi mko hapa, lichukueni hili kama ajenda.

“Hakikisheni watoto hawa walemavu, yatima, wanaoishi mazingira magumu na wenye mahitaji maalum, wasiwe wanafikiwa tu kipindi cha Ramadhani, iwe ni utaratibu wa kila siku katika maisha yao yote. Halmashauri ziratibu mwenendo wao, mahitaji yao, huduma zao, ili watoto hawa tuwalee.

“Hawa ndio Watanzania ambao baadaye watakuwa viongozi wa taifa hili, kwahiyo Mamlaka za Serikali za Mitaa, jifunzeni kutoka kwa NMB, namna ya kushiriki kikamilifu kutambua vituo na kuvihudumia,” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Meya wa Dar es Salaam, Omar Kumbilamoto.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kulia), akitoa mchango kwaajili ya maandalizi ya Futari kutoka kwa NMB kwa watoto wanaolelewa katika Kituo cha kulelea Watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Umrah Orphanage wakati hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB. Wa pili kulia ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Juma Kimori.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ruth Zaipuna, alitoa salamu za shukrani kwa Waziri Mkuu kwa kuhudhuria hafla hiyo, akiwashukuru pia wateja, wadau na viongozi wote waliotikia mwaliko wa taasisi yake kujumuika pamoja.

“Katika kila Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tumekuwa na utamaduni huu wa kupata futari ya pamoja na wateja wetu, wadau, viongozi na waalikwa wengine kama ishara ya upendo, umoja, mshikamano. Ujio wenu nyinyi wote unathibitisha kuwa nyie ni familia ya NMB.

“Pamoja na futari hii, lakini mwaka huu tutakabidhi misaada kwa watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu. Tuna vituo vitatu hapa vyenye watoto takribani 200, ambavyo tunaenda kuvipa zawadi za mfungo ili wakitoka hapa wakaendelee kuufurahia mwezi wa Ramadhani na Sikukuu ya Idd,” alibainisha Kimori.

Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk Edwin Mhede, alisema umuhimu wa majumuiko ya namna hiyo ni kujenga jamii ya watu wenye Hofu ya Mungu, watu ambao wanahitajika sana katika kukuza Uchumi wa Nchi na ustawi wa taasisi kama NMB.

“Afisa Mkuu wa Fedha tayari ameshazungumza kwa kina, kwamba pamoja na ibada ya futari, NMB inaenda kuwashika mkono wahitaji ambao tumeambatana nao hapa. Wito wetu kwa jamii ni kuendelea ‘kubenkika’ na NMB inayotumia kaulimbiu ya Karibu Yako, ili kutanua familia hii,” alisema Dk Mhede.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!