May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ndugai aimwagia sifa Simba, atamba kuikata ngebe Yanga Julai 3

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameipongeza klabu ya Simba kwa kufikia hatua ya robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara baada ya kuondoshwa kwenye michuano hiyo na Kaizer Chiefs. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Simba Jumamosi ilishuka Uwanjani kwenye mchezo wa robo fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Kaizer Chiefs na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, na kuondoshwa nje ya michuano hiyo mara baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-0 kwenye mchezo wa awali uliofanyika nchini Afrika Kusini.

Akiongea leo Bungeni Jijini Dodoma,Ndugai ameipongeza klabu ya Simba kwa kuitoa Tanzania kimasomaso kwa kufikia hatua ya robo fainali na kutaka watani zao klabu ya Yanga waige mafanikio hayo na sio tu kuishia kucheza ligi ya ndani.

“Kama Bunge lazima tupongeze kwa timu yetu ya Simba, kututoa kimasomaso kwa kuweza kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, si haba na wale rafiki zetu wengine wajitahidi kidogo badala ya kucheza ligi tu hapa hapa waige wasiogope,” alisema Ndugai.

Aidha Ndugai aliipongeza timu ya Namungo FC kwa kuingia kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kuingia hatua ya makundi, na kuwarushia kijembe waliokuwa wanawashangilia wageni walipokuwa wakicheza na Simba watapata majibu yao tarehe 3 Julai, 2021.

“Hata Namungo wamejitahidi ni mara ya kwanza wameingia mashindano makubwa, sasa wengine mpo wapi? Badala yake tunaishia kushangilia wageni na mwisho wa haya ni tarehe 3 Julai ndio majibu yatapatikana,” aliongeza Ndugai.

Ikumbukwe tarehe 3 Julai, 2021 ndio siku iliyopangwa na bodi ya ligi kupigwa kwa mchezo kati ya Simba na Yanga baada ya kuahilishwa kuchezwa tarehe 8 Mei, 2021 kutokana na mabadiliko ya ratiba.

Kwa sasa Simba inarejea kwenye mashindano ya ndani baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo siku ya Jumatano tarehe 26 Mei, 2021, itashuka uwanjani kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe Shirikisho (Azam Federation Cup) dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika hatua nyingine Spika huyo wa Bunge amewapongeza wizara pamoja na viongozi wa klabu hizo kwa mafanikio makubwa waliyopata na kutaka wajipange zaidi mwakani kwenye michuano hiyo.

error: Content is protected !!