June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yatoa muongozo matibabu ya wazee

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imeagiza hospitali, zahanati na vituo vya afya vya umma, viweke watu maalum kwa ajili ya kuwahudumia wazee. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Agizo hilo limetolewa jana tarehe 23 Mei 2021, na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma.

Dk. Gwajima aliagiza watu hao wawe na sare maalum, zitakazowawezesha wazee kuwatambua.

“Kila kituo lazima kiwe na nesi mmoja, afisa ustawi wa jamii pamoja na daktari aliyepangwa zamu na lazima wavae sare, ambayo itamtambulisha na imeandikwa ‘Mzee ni Tunu, Tunakupenda, Tunakuheshimu’,” alisema Dk. Gwajima.

Aidha, Dk. Gwajima aliagiza vituo hivyo kuweka mabango yanayoelekeza mahali wazee watapata huduma.

“Lazima kuweka mabango yanayomuelekeza au kumuongoza mzee, wapi atapata huduma anazozihitaji na ambayo yameandikwa “Mpishe Mzee apate huduma kwanza,” alisema Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima alisema wizara yake imeanza kufanya ufuatiliaji wa maelekezo hayo, ili kuboresha huduma za matibabu kwa wazee, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Aidha, Dk. Gwajima alisema wizara hiyo iko mbioni kutengeneza muongozo rasmi, ambao utaweka uwiano wa utekelezaji maagizo hayo, katika hospitali zote nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dk. Vivian Wonanji, alisema idara yake imeandaa mkakati wa utoaji huduma kwa wazee wa miaka kumi. Ifikapo Juni 2021 itaanza kuandaa mpango wa utekelezaji wake.

Dk. Wonanji alisema mpango mkakati huo utakuwa na mambo mbalimbali, yakiwemo kuzalisha wataalam wa kutoa huduma za wazee.

“Kama tunavyofahamu wazee wanahitaji mambo mengi, ikiwemo masuala ya lishe na utengamao. Hivyo mkakati huo utakua na maono muhimu, ambayo yatasaidia kuboresha huduma za wazee nchini,” alisema Dk. Wonanji.

error: Content is protected !!