May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ndugai aeleza kinachowaangusha wabunge kurejea bungeni

Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa Bunge Tanzania

Spread the love

 

JOB Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania, ametahadharisha wabunge, wasikae kimya vinginevyo watashindwa kurudi bungeni mwaka 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kiongozi huyo wa Bunge ameonesha hofu hiyo jana Alhamisi tarehe tarehe 4 Februari 2021, katika mjadala wa wabunge kuhusu Hotuba ya Rais John Magufuli wakati akifungua shughuli za Bunge la 12.

Rais Magufuli alifungua Bunge hilo tarehe 13 Novemba 2020, jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa mjadala huo, Spika Ndugai amesema, wabunge wengi wanashindwa kurudi bungeni kutokana na kutochaguliwa tena na wananchi wao.

Na kwamba, ni adhabu yao kwa kushindwa kutatua changamoto ya ubovu wa miundombinu hasa barabara na madaraja.

“Na wabunge wengi wanakuwa hawarudi, adhabu zao kubwa ni barabara, wananchi wanasema tukuchague daraja letu limevunjika, miaka 10 halijatengenezwa, mbunge gani wewe? Wanaanguka wanakuja wapya, wanaanguka tena,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amewatahadharisha wabunge hao, kwamba kama watashindwa kuwabana Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), katika kutatua changamoto hiyo, hawatarudi bungeni.

“Sasa safari hii hebu tulishike hili kama wabunge, vinginevyo na nyie hamtarudi. Nyie chekeni na TARURA,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amesema, kama wabunge hao hawatapaza sauti zao bungeni kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo, kila mwaka mijadala hiyo itaibuka.

“Lazima tufike mahali tukiamua kuhusu jambo hili, sababu tusipofanya hivyo hata mwakani michango itakuwa hivi, sasa itakuwa muda wa wabunge kuliongelea jambo hilo hilo moja kila siku. Inakuwa haipendezi,” amesisitiza Spika Ndugai.

Alitoa ushauri huo kwa wabunge baada ya wabunge kadhaa akiwemo Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe (CCM), wameeleza mateso wanayopata katika majimbo yao kutokana na changamoto hiyo.

Akichangia mjadala huo, Askofu Gwajima amesema “hakuna mateso tuliyonayo wabunge kama Tarura kukosa pesa kule mkoani, ni ngumu sana.”

Askofu Gwajima amesema, haingii akilini kuona Tarura yenye mtandao mrefu wa barabara kutendengewa fedha kidogo, wakati Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), yenye mtandao mfupi ikitengewa fedha nyingi.

“Haileti sense (mantiki) ukiona kwamba mtandao wa baraba za Tarura ni takribani km 130,000 na mtandao wa barabara za Tanroad ni km 40,000. Kwa nini mpaka leo TARURA anapewa asilimia 30 na Tanroad asilimia 70” amehoji Askofu Gwajima.

Askofu Gwajima ametolea mfano Jimbo la Kawe lenye kilomita 1,463, akisema kwamba Tarura ina uwezo wa kutengeneza kilomita 120.

“Jimbo la Kawe likiwa na kilomita 1,463 ni sawa na kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma, lakini zote ziko Kawe, nilipowatembelea Tarura wana hela za kutengeneza kilomita 120, ina maana kuna kilomita 1,300 ambazo haziwezi kutengenezwa,” amesema Askofu Gwajima.

Ramadhani Abeid Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), ameshauri Tarura ivunjwe kama haipewi fedha za kutosha.

“Mimi hotuba yangu ijielekeze kwenye kushauri, suala la Tarura ni msiba ukienda vijijini hakuna barabara ni mapalio. Tumechoka kupita kwenye mapalio, tunashauri kama hii Tarura haipewi fedha, ifutwe,” ameshauri Ighondo.

Akikazia hoja hiyo ya Tarura kuongezewa fedha za uendeshaji majukumu yake, Spika Ndugai ameshauri serikali kuongeza katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha, ili kero ya ubovu wa barabara imalizike.

“Wazo la kwamba Tarura waongezewe fedha, wenzetu wa serikali ni wazo limesemwa miaka mingi na kila mtu anaongelea jambo hili. Basi iongezewe Tarura lakini lakini pafanyike change (mabadiliko), hatuwezi kuendelea hivi,” amesema Spika Ndugai na kuongeza.

“Ni jambo la kulitazama kwenye bajeti hii inayokuja, ni kuangalia hiyo fomula (kanuni) kama iko kwenye sheria au ilikuwa inahitajika kuangaliwa, kwa kweli ni kilio cha miaka mingi.”

error: Content is protected !!