Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Nape ataka elimu bure ifumuliwe, Silinde amjibu
Habari za Siasa

Nape ataka elimu bure ifumuliwe, Silinde amjibu

Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama (CCM)
Spread the love

 

MBUNGE wa Mtama mkoani Lindi, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, ameishauri Serikali ya Tanzania, ifanyie marekebisho sera ya elimu bila malipo, ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezwaji wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Nape ametoa ushauri huo leo Jumatano tarehe 31 Machi 2021, wakati anauliza maswali ya nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu, bungeni jijini Dodoma.

Akieleza changamoto zilizopo katika sera hiyo, Nape amesema, vigezo vyake vinafanya baadhi ya shule hasa zenye idadi ndogo ya wanafunzi, kupata fedha kiduchu za ruzuku ikilinganishwa na mahitaji yake.

“Baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali kutoa elimu msingi bila malipo kwa miaka mitano mfululizo, kuna changamoto ilijitokeza kwenye eneo hili.”

“Na moja ya eneo kubwa ni kwamba vigezo vinavyotumika kupeleka fedha vinasumbua hasa shule ambazo zina wanafunzi wachache,” amesema Nape.

Nape amehoji “Shule zinawafunzi wachache wakati baadhi ya mahitaji hasa ya utawala yanafanana, je, Serikali haioni imefika wakati wa kupitia upya vigezo hivi na kuona namna bora ya kupeleka fedha hasa maeneo ya utawala ili kutaua tatizo hili?”

Changamoto nyingine aliyoitaja Nape ni sera hiyo kutoijumuishi elimu ya kidato cha tano na sita, hali inayowafanya wanafunzi husika kukosa elimu inayotolewa na Serikali.

“Elimu msingi kwa tafsiri iliyokuwa inatolewa ni kuanzia chekechea hadi kidato cha nne, hapa kuna kidato cha tano na sita ambacho haina fedha,” amesema.

“Elimu ya juu kuna mikopo, je Serikali haioni ni wakati sasa umefika kuhusisha kidato cha tano na sita kwenye elimu bila malipo ili nao wapate elimu ambayo inatolewa na Serikali?” amehoji Nape.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, David Silinde

Akijibu maswali ya Nape, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, David Silinde, amesema Serikali imepokea changamoto ya baadhi ya shule kupata fedha ndogo na kwamba itaishughulikia kulingana na bajeti.

“Ni kweli alichoeleza mbunge kwamba, Serikali ina vigezo vyake ikiwemo idadi ya wanafunzi na ndio mfumo tunaotumia kupeleka ruzuku kwenye shule zote nchini.”

“Na bahati mbaya sana, kwenye shule ambazo wanafunzi wachache tumekuwa tunapeleka fedha kulingana na mahitaji na idadi iliyopo,” amesema Silinde.

Silinde amesema “ndio maana nimeeleza kwenye swali langu la msingi, kulingana na bajeti na mahitaji tutaendelea kutenga fedha, naomba niipokee hiyo changamoto na tutaifanyia kazi.”

Kuhusu kidato cha tano na sita kujumuishwa katika sera hiyo, Silinde amesema Serikali italifanyia kazi suala hilo.

Chuo Kikuu cha Dodoma

“Kuhusiana na wanafunzi elimu ya kidato cha tano na sita ambayo ameeleza hawahusiki na elimu bila malipo, ngoja niipokee sababu ni mfumo wa kisera. Tutaifanyia kazi tuone mahitaji yake na mazingira,” ameahidi Silinde.

Aidha, Silinde amesema mbali na Serikali kutoa elimu ya msingi bila malipo, imeendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya utoaji elimu, ikiwemo kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni na maabara.

“Serikali ilikuwa na nia njema kuanzisha elimu bila malipo, na kutokana na hiyo nia njema nyote mnajua moja ya jitihada kubwa ya Serikali ilikuwa ni kuboresha miundombinu hususan maeneo ya shule nyingi zinakosa uhitaji,” amesema Silinde

“Na wabunge ni mashahidi, Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni pamoja na maabara.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

error: Content is protected !!