RAIS Mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, anaendelea kupatiwa matibabu chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari, huku familia ikiwaomba Watanzania wamuombee ili afya yake iimarike arudi kwenye hali ya kawaida. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Maendeleo ya afya ya Rais Mwinyi anayepatiwa matibabu kwa maradhi ya kifua, imetolewa jana Alhamisi na aliyekuwa katibu wake, Dk. Abdallah Makame, akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam.
Dk. Makame alisema kwa sasa madaktari wanaomhudumia wameona hakuna haja ya kiongozi huyo kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
“Anaendelea kupata matibabu na baadhi ya wakati anakuwa na uangalizi wa karibu sana wa madaktari na wamesema kwamba wataendelea kumpa matibabu kwa hapa hakuna haja kwa sasa ya kumsafirisha labda kama watakuja kuona kuna haja ya kufanya hivyo,” alisema Dk. Makame na kuongeza:
“Na umri umesogea kidogo, mimi cha kusema tu tumuombee mzee wetu tumfanyie dua, tumuombee aweze kuimarika afya yake na aweze kutoka katika hali hiyo ya maradhi aungane na sisi tena tuendelee kupata faida kwake.”
Leave a comment