July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mzee akataliwa kijijini kwa ubabe, kupora mashamba

Spread the love

WANANCHI wa Kijiji cha Yakobi, Halmashauri ya Mji wa Njombe wamemkataa mwananchi mwenzao aliyefahamika kwa jina la mzee Gerhad Makinda kuishi kijijini hapo kutokana na tabia yake ya kupora mashamba kwa wananchi wenzie na kuwatolea lugha mbaya pindi wanapomhoji kuhusu vitendo hivyo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika taarifa ya Kijiji iliyosomwa na Mtendaji wa Kijiji hicho imeelezwa kuwa mwananchi huyo amekuwa si muungwana.

Amedai amekuwa akichoma mashamba ya watu ambayo anataka kuyapora, kulisha mifugo yake katika mashamba ya wakulima, mbwa wake kung’ata mifugo ya wananchi na yeye kukataa huku akiwatolea lugha za kuudhi.

Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa akiwa ziarani kijijini hapo alimuita Mzee Makinda kujibu tuhuma hizo ambapo pamoja na mambo mengine Mzee huyo alidai kuwa amebambikiwa tuhuma hizo.

Amesema tuhuma hizo zinazungumzwa juu yake kutokana na ukweli ambao huwa anauzungumza kwa viongozi wasio na maadili.

Amedai kuwa baadhi ya viongozi wa kijiji hicho nao wamemia na kupasua mbao kwa nguvu katika shamba lake

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alitaka kuteua baadhi ya wazee maarufu kijijini hapo ili kukaa na Mzee Gerhad Makinda ili kujua ni kwanini analalamikiwa na wananchi lakini cha kushangaza wazee wote waliochaguliwa walikataa kukaa na mhusika kwa madai kuwa hawawezi kuelewana naye kulingana na tabia yake.

Baada ya kuona hali hiyo Mkuu wa wilaya amesema kuwa mwananchi huyo ataitwa mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ili ahojiwe ni kwanini anafanya vitendo hivyo vinavyochochea migogoro huku akiwataka wananchi kijijini hapo kuacha kuchukua hatua mkononi.

error: Content is protected !!