JESHI la polisi mkoani Songwe linamshikilia Mwalimu Baraka Mwashihuya mkazi wa kitongoji cha Tazara – Mamlaka ya mji mdogo wa Mlowo wilayani Mbozi mkoani Songwe, pamoja na mkewe ambaye ni mwalimu wa sekondari ya Msense kwa tuhuma ya kumficha mtoto wa miaka nane chumbani. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).
Akizungumza tukio hilo jana tarehe 31 Januari 2024, Bibi wa mtoto huyo, Sevelina Lwesye amesema tarehe 29 Januari mwaka huu mjukuu wake aitwaye Bradness Korneli Mwasote (8) hakuonekana nyumbani ndipo walipoanza kumtafuta pasipo mafanikio.
Amesema ilipofika jioni waliitaarifu serikali ya kijiji ambao waliungana nao kumtafuta pasipo mafanikio lakini walipata taarifa kwa msamaria mwema mmoja aliyewaonesha nyumba ya Mwalimu Mwashihuya.
Amesema baada ya kuoneshwa alipo mjukuu ndipo walipolitaarifu jeshi la polisi ambao walifika na kupekuwa chumba kimoja baada ya kingine na kumkuta mtoto huyo amefunikwa na blanketi mbili pamoja na godoro.
Amesema polisi walimtoa mtoto akiwa amedhoofu kutokana na njaa ya kutokula kwa siku nzima.
Baba wa mtoto huyo Korneli Mwasote ambaye ni mchungaji wa kanisa la TAG Mbeya amesema alipatwa na mshangao juu ya tukio hilo lakini anamshukuru Mungu kwa kuwa mtoto wake amemkuta akiwa salama.
Katibu wa Mwenyekiti wa kitongoji cha Tazara, Smith Muyombe licha ya kuthibitisha uwepo wa tukio hilo, amesema hilo ni tukio la pili kutokea kwani mwishoni mwa mwaka jana alikamatwa mtu mmoja aliyeiba mtoto wa miezi minne.
Amesema mtu huyo alikamatwa na sasa yupo gerezani. Ameongeza na kutokana na hali hiyo zaidi wananchi 71 wamejiorodhesha wakitaka watuhumiwa wanaoiba watoto wahamishwe katika mtaa huo.
Kaimu kamanda wa polisi mkoani Songwe, Gallus Hyera licha ya kuthibitisha uwepo wa tukio hilo, amesema atalizungumzia kwa kina.
Leave a comment