May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mvutano chanjo ya Corona wamuibua Rais Samia, atoa msimamo

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewatoa hofu Watanzania dhidi ya chanjo ya ugonjwa wa corona, akisema kwamba ni salama kwani inasaidia kupunguza vio vinavyotokana na ugonjwa huo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumapili, tarehe 22 Agosti 2021, akipokea kombe la ushindi la michuano ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23 (CECAFA Challenge Cup 2021), Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amewaomba Watanzania wapuuze maneno yanayotolewa na baadhi ya watu wanaodai kwamba chanjo hiyo ina madhara kwa afya ya binadamu.

“Kuna mwanangu aliimba huwezi kushindana na wanadamu mwenye kinywa, mwenye kinywa atasema anayotaka kusema. Lakini ukweli utabaki palepale kwamba chanjo hizi zinasaidia kupunguza maumivu na vifo vya watu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia aliyezindua zoezi la utoaji chanjo hiyo tarehe 28 Julai 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam, amesema hawezi kuipeleka jamii yake kwenye hatari, kufuatia uamuzi wake wa kuruhusu chanjo hiyo kutolewa kwa wananchi.

“Kwa hiyo chanjo hatusemi ni kinga kabisa, lakini hata ikikupata inakupata polepole. Risk ya kufa kwa wingi inapungua, niwaombe wana michezo mkitaka kuendelea na michezo vizuri chanjeni. Mimi mama yenu, mkuu wenu sitaipeleka jamii yangu kwenye hatari hata siku moja,” amesisitiza Rais Samia.

Akizungumza na wadau wa michezo waliohudhuria hafla hiyo, Rais Samia amewaomba wajitokeze kwa wingi kupata chanjo ya corona, ili kulinda afya zao.

“Suala la chanjo ni muhimu sana, wanamichezo kama hamjachanja naomba sana mkachanje, tulianza kuchanja tukasema tutahanja makundi maalumu yaliyo kwenye hatari na sasa tunaendelea. Lakini wanamichezo mnasafiri hapa na kule na kila mnakopita test za covid-19 zinawasubiri,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“ Ukichanja kwanza utakua na ushahidi kwamba umeachanja, lakini pili hata kama maradhi yakikupata hayaji kwa nguvu kama utakavyokuwa haujachanja.”

Mvutano kuhusu chanjo ya Korona uliibuka baina ya Mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima na Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, baada ya mbunge huo kupinga hadharani utolewaji wa hafua hiyo.

Askofu Gwajima alipinga chanjo hiyo kwa madai kwamba hakuna utafiti rasmi uliofanyika na kuonesha kama ina madhara au lah, huku akiitaka Serikali iitishe mdahalo wa wazi ili wataalamu wa afya waijadili na kutoa maamuzi kama inafaa kutolewa kwa wananchi.

Kufuatia msimamo wake huo, Waziri Gwajima aliviagiza vyombo vya dola vimhoji Askofu Gwajima ili athibitishe madai yake ya kwamba kama chanjo hiyo si salama.

error: Content is protected !!