November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mshindi Maalim Seif CUP apatikana

Spread the love

 

TIMU kutoka Wete Kaskazini Pemba imenyakua ubingwa wa Kombe la Maalim Seif linalojulikana kama ‘Maalim Seif CUP’ katika fainali iliyochezwa jana tarehe 22 Oktoba, 2021 kwenye Uwanja wa Madungu Polisi Chakechake Pemba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pemba … (endelea).

Mashindano hayo maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa nguli wa siasa Zanzibar na Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad yalishirikisha timu 18 zote kutoka Pemba.

Miongoni mwake Timu kutoka Wete Kaskazini na Mkoa wa Kusini Pemba ziliingia fainali na Timu ya Wete Kaskazini ikaibuka kidedea na kujinyakulia zawadi ya kombe, jezi pea tatu na mipira miwili.

Mshindi wa pili Timu ya Mkoa wa Kusini Pemba na mkoa wa kichama Mkoani ilipata zawadi ya jezi pea mbili na mipira miwili.

Mshindi wa tatu alitokea Chake Chake huku mshindi wa nne akitokea Jimbo la Chambani ambayo ilipata zawadi ya jezi na mpira.

Akikabidhi zawadi kwa washiriki na washindi wa michuano hiyo, Makamo Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Zanzibar, Khadija Anwar Mohammed alisema Mashindano hayo niya kwanza kufanyika baada ya kifo cha Marehemu Maalim Seif kufariki Dunia mapema mwaka huu.

Khadija ambaye pia alikuwa mgen rasmi katika fainali hizo, alisema timu zote 18 zilizoshiliki mashindano hayo zimepata zawadi ya mpira mmoja mmoja.

“Madhumuni makuu ya shughuli hii ya leo ni kukumbuka Siku ya kuzaliwa kwa Kiongozi wetu kipenzi cha Wazanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye aliwaunganisha vijana jamii kwa ujumla wake.
Tunaahidi kuendelea kuenzi siku hii kila mwaka kwakuwa hii ni siku kubwa na maalum kwetu.

“Shukrani zangu nakwa niaba ya Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo tunawashukuru timu zote zilizoshiriki, wanachama pamoja na wote waliounga mkono mashindano haya” alisema Khadija.

Maalim Seif ambaye alitokea kuwa mwamba wa siasa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla alizaliwa tarehe 22 Oktoba, mwaka 1943 na kufariki dunia tarehe 17 Februari, 2021.

error: Content is protected !!