December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba amaliza kazi, amng’oa Maalim Seif

Spread the love
HATIMAYE Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francies Mutungi, amekamilisha kazi aliyotumwa. Anaripoti Hamis Mguta … (endelea).

Amempachika Halifa Suleiman Halifa kwenye cheo cha Katibu Mkuu wa chama hicho, kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad. 

Maalim Seif, mwanasiasa nguli Visiwani, ametangazwa kuvuliwa wadhifa huo na kufukuzwa uwanachama kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Maamuzi hayo yanayotajwa na wachambuzi kuwa ni kinyume cha sheria, yamefanyika leo tarehe 16 Machi 2019 na  mkutano wa Baraza Kuu la taifa la chama hicho.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo, Halifa amesema, “wale watu walioingia kwenye chama kwa ajili ya chama na kuwatafutia watu maendeleo, wataendelea kubaki.”

Amesema, Makao Makuu ya CUF yaliyopo Zanzibar siyo mali ya Maalim Seif. Amedai kuwa pamoja na kwamba kwa sasa yeye ndiye anayeitumia ofisi hiyo, lakini wao wataichukua.

Amemtaja Maalim Seif kama kiongozi wa kawaida sana na hana sifa zaidi ya ubinaadamu hivyo alikuwa na upungufu wake katika kipindi chake cha uongozi.

Mfumo wa kumpata Katibu Mkuu wa CUF ya Lipumba, umefanyika kupitia marekebisho ya Katiba, ambapo kabla ya hapo, kingozi wa ngazi hiyo alikuwa akichaguliwa na mkutano mkuu wa taifa.

Katika mabadiliko ya sasa ambayo yanamfanya katibu mkuu kuwa “mtumwa wa mwenyekiti,” kiongozi huyo anapendekezwa na mwenyekiti wake na kisha Baraza Kuu kumuidhinisha.

Naye Magdalena Sakaya alichaguliwa kuwa Naibu Katibu Mku Bara na Fakhi Suleima Hatibu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Uchaguzi huo umefanyika wakati ndani ya chama hicho kukiwa na mgogoro wa kimamlaka uliodumu kwa miaka mine sasa na kukiwa na zuio la Mahakama.

Tayari kambi ya Maalim Seif imeeleza kutotambuwa mikutano yote iliyoitishwa na Prof. Lipumba na genge lake.

Maalim Seif anasema, Prof. Lipumba siyo mwanachama wa chama hicho na hivyo hana sifa ya kuwa mwenyekiti.

“Lipumba alitangaza hadharani kujiuzulu uenyekiti wa CUF katikati ya mwaka 2015 na baadaye Baraza Kuu la Taifa likamfukuza uwanachama. Leo mtu wa aina hiyo, anawezaje kuwa mwanachama na kiongozi wa chama chetu,” ameeleza Maalim.

error: Content is protected !!