April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yakaripia wawekezaji waliouwa viwanda

Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Mazingira

Spread the love
SERIKALI imesema, iko mbioni kutaifisha viwanda vyote ilivyovibinafsisha kwa watu binafsi, lakini wameshindwa kuviendeleza. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Injinia Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, ameiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, kuwa “serikali haitavumilia muwekazji aliyeshindwa kuendesha kiwanda alichouziwa.”

Naibu waziri alitoa kauli jana jijini Arusha wakati Kamati hiyo ilipotembelea kiwanda cha Bia cha Tanzania Breweries Limited (TBL).

Alisema, “serikali ilipoamua kubinafsisha viwanda vyake, ilifanya hivyo ili kuleta ufanisi. Haikubinafsisha viwanda ili kugeuzwa maghara ya kuhifadhia mizigo; na au kufugia mbuzi ama kuviuwa.”

Naibu Waziri Manyanya amesema, watu wote waliokabidhiwa viwanda kwa njia ya ubinafishaji, lakini wakashindwa kuviendeleza, watanyang’anywa viwanda hivyo na kukabidhiwa watu wengine au vitarejeshwa serikalini.”

Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, ipo jijini Arusha kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo na kutembelea idara na taasisi za serikali zilizoko chini ya wizara hizo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ni Murad Sadiq, mbunge wa Mvomero, mkoani Morogoro.

Kauli ya waziri ilitokana na maombi ya uongozi wa kiwanda cha TBL kukadhiwa eneo ambalo lilikuwa linatumiwa kwa ajili ya kiwanda cha nguo cha Kiltex.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kiwanda hicho kiliuzwa kwa mfanyabiashara mmoja mashuhuri jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake hiyo, Injinia Manyanya alisema, “serikali inapaswa kuhakikisha viwanda vilivyopo vinaimarishwa na vingine vinajengwa ili kutoa ajira kwa wananchi.”

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, walisisitiza kuwa ni sharti serikali ihakikishe kuwa eneo hilo linakabidhiwa kwa kiwanda.

error: Content is protected !!