November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mkazi Dar ajishindia pikipiki ya NMB Bonge la Mpango

Spread the love

 

MSHINDI wa Droo ya Nne ya Msimu wa Pili wa Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde inayoendeshwa na Benki ya NMB ‘NMB Bonge la Mpango – 2merudi Tena,’ Richard Jeremiah Iranga, amekabidhiwa pikipiki ya miguu mitatu aina ya Skymark yenye thamani ya Sh.45 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Iranga, ambaye ni mfanyabiashara wa mazao na mkazi wa Goba, wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam, amekabidhiwa pikipiki hiyo leo Jumatatu, tarehe 15 Novemba 2021 na Meneja wa NMB Tawi la Mlimani City, Deogratius Kawonga, hafla ya makabidhiano ikifanyika Viwanja vya Stendi ya Daladala ya Mawasiliano ‘Simu 2000.’

Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi hiyo, Kawonga alisema NMB Bonge la Mpango ni kampeni ya miezi mitatu, inayohamasisha utamaduni chanya wa kuweka akiba, ambako kila wiki washindi 10 huzawadiwa pesa taslimu Sh.100,000, kila mmoja, huku wengine wawili wakitwaa pikipiki ya Skymark ya Sh.4.5 milioni (moja kwa kila mshindi).

Wiki 12 za droo hiyo, zitazalisha jumla ya washindi 170 watakaozoa zawadi zenye thamani ya Sh.237 milioni, kigezo cha ushiriki kikiwa ni kufungua akaunti na kuweka angalau Sh. 100,000 ama mteja mwenye akaunti kuweka akiba isiyopungua kiasi hicho.

Kawonga aliwataka wateja wa benki hiyo kuendelea kujiwekea akiba ili kujiongezea nafasi za kushinda zawadi hizo, huku akiwataka wasio na akaunti NMB kuchangamkia Bonge la Mpango kwa kufungua akaunti ikiwa na kianzio kinachompa mteja haki ya kushiriki kampeni hiyo na kutwaa zawadi.

Kwa upande wake, Iranga alikiri kufurahia zawadi hiyo, ambayo kwake ni zaidi ya mtaji, kwani itaenda kumpunguzia gharama za usafirishaji wa mazao ya biashara kutoka sehemu moja kwenda nyingine, ambao ulikuwa unamgharimu pesa nyingi na kumpa wakati mgumu.

“Wito wangu kwa Watanzania ni kuendelea kuchangamkia huduma za NMB, ambazo zinakuja na fursa kibao. Mimi wakati naweka akiba sikufikiria kuwa naweza kuibuka mshindi, kwa hiyo hii ni nafasi ya wazi kwa kila mmoja wetu, kikubwa bahati yako tu,” alisisitiza Iranga, ambaye ni mteja mwenye akaunti katika Tawi la Mlimani City.

Aidha, katika droo ya tano ya NMB Bonge la Mpango iliyochezeshwa Ijumaa Novemba 12, Evelyn Ndowo wa NMB Tawi la Clock Tower na Derick Kazinduki wa Tawi la Sengerema, waliibuka washindi wa pikipiki mbili za Skymark, huku washindi 10 wa pesa taslimu wakitangazwa pia.

Katika droo hiyo, wateja 10 walizoshinda jumla ya Sh.1 milioni na matawi yao kwenye mabano ni: Chiku Humbi (Kahama), Christina Msangi (Tunduma), Mariam Lumba (Morogoro Road) na George Mwendi (Bunge).

Wengine ni Penuel Mwanry (Dodoma), Atui Mwaipyana (Wami), Daud Masana (Bagamoyo), Fredrick Zacharia (Clock Tower), Joseph Mwingira (Mbinga) na Magesa Mwendwa (Mlimani City).

error: Content is protected !!