December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mawakili wa Mbowe, jamhuri wavutana kuenguliwa shahidi

Spread the love

 

MAWAKILI wa utetezi na jamhuri katika kesi ya makosa ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, wameonesha umwamba wa kujenga hoja katika pingamizi la kukataliwa kwa shahidi wa jamhuri. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pingamizi hilo, liliwekwa Ijumaa iliyopita tarehe 13 Novemba 2021 katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano jijini Dar es Salaam mbele ya Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo.

Upande wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, waliweka pingamizi la kumkataa shahidi wa pili wa Jamhuri, askari polisi Ricardo Msemwa, baada ya kukutwa akiwa na simu, shajala, karatasi na kalamu akiwa kwenye kizimba cha kutolea ushahidi.

Leo Jumatatu, tarehe 15 Novemba 2021, mawakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya na Peter Kibatala wamewasilisha hoja za kumpinga shahidi huyo huku upande wa mashtaka wakiweka hoja zao mezani wakidai pingamizi hilo halina uzito na litupiliwe mbali.

Mtobesya amedai shahidi huyo amekiuka kwa kukutwa na vifaa hivyo bila kibali cha mahakama.

“Suala la kutoa ushahidi linaongozwa na sheria namba sita ya sheria zetu ambayo ni Sheria ya Ushahidi kama ambavyo imefanyiwa marekebisho mwaka 2016.”

“Ukisoma Sheria ya Ushahidi na PGO inaonesha shahidi ambaye atakuwa ni Polisi, kwa sasa tunamzungumzia ambaye yupo kizimbani atakuwa na nyaraka zozote endapo tu ataruhisiwa na Mahakama,” amedai Mtobesya.

Amedai “kama ruhusa inatoka ni pale anapotakiwa ku- refresh memory tu. Tunayesema kwa kifungu cha 168 (1) ya sura ya 6 ya Sheria ya Ushahidi na PGO namba 282 (7) na aya ya saba paragraph A, B na C. Aya ya saba inasema kwamba afisa wa polisi anaweza kuwa na nyaraka baada ya kupata ruhusa ya Mahakama.”

Mtobesya amedai ikitokea kuna umuhimu wa kiambatanisho au nyaraka kuingia mahakamani utaratibu utafuatwa na ambao umetajwa katika Sheria ya Ushahidi na katika PGO 282(7).

“Kutokana na utaratibu huo, shahidi alipaswa kuomba ruhusa ya Mahakama, na kibaya zaidi ikiwa wazi wakati mahakama ikiendelea. Tunasisitiza hizo tataratibu lazima zifuatwe ili washitakiwa wapate haki yao wakati wa cross examination,” amedai Mtobesya na kuongeza:

“Ukienda sasa Sura 20 ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kwenye kifungu cha 264 kinaonesha nguvu ya mahakama hii. Kwa vifungu hivyo viwili vya sheria hizo mbili kama ambavyo zimefanyiwa marekebisho mwaka 2019.

“Kama nilivyosema kwenye utangalizi, kwamba kitendo cha shahidi kukutwa na ‘diary’ hasa ikiwa wazi wakati mahakama inaendelea, shahidi aonekane hafai na hakidhi, na tutaieleza mahakama kwanini tunasema hivyo.”

Wakili huyo ameiomba mahakama kuangalia uamuzi itakaoutoa utakavyokwenda kushuhudia mamilioni ya mashahidi wakiingia na ‘diary’ kwenye vizimba na kuwanyima haki washtakiwa.

Kibatala anayeongoza jopo la mawakili wa utetezi, ameunga mkono hoja za Mtobesya akisema, ili shahidi aruhusiwe kuwa na nyaraka au kitu kingine katika kizimba cha shahidi lazima awe na ruhusa ya mahakama na au upande wa pili uwe na haki ya kutumia nyaraka au kitu hicho.

Kibatala amedai, upande wao unaiomba mahakama hiyo ifanye zoezi la kuangalia shajala aliyokutwa nayo shahidi kizimbani ijumaa iliyopita ili kubaini kama inaruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

“Test ambayo tunaiomba mahakama itumie ni kwenye chumba cha mitihani, ingalie je, unapopatikana na nyaraka isiyoruhusiwa, je, umepatikana na un-authorised material. Kama jibu ni ndiyo basi shahidi amekosa sifa,” amedai

Kibatala amesema “hiyo ‘diary’ aliyokuwa nayo ni kwamba ipo katika Mahakama na imetoka kwenye kizimba moja kwa moja kwenye mikono ya shahidi, na haijapitia kwingine kwamba inaweza kuwa siyo, na kwamba nasema muda ambao ilichukuliwa diary alikuwa bado kwenye kizimba na kesi ikiendelea.”

Kibatala amedai, shahidi akitoa ushahidi wake sehemu nyingine ushahidi wake unakuwa sio halali.

“Wakili Mtobesya amekurejesha kifungu cha 127 ambapo unakuwa na nguvu ya kumuondoa shahidi. Ni kweli tunakiri mle hakuna neno shahidi, isipokuwa Bunge limeweka maneno kwamba na vingine vinavyofanana na hivi…”

“Mheshimiwa Jaji tunakurejesha pia kwenye kifungu cha 62, kwamba shahidi atoe ushahidi ndani yake, akitoa kwingine ushahidi unakuwa siyo direct oral evidence,” amedai Kibatala.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha hoja zao kuhusu suala hilo, akianza Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, amedai pingamizi hilo halina mashiko kwa kuwa wakati upande wa utetezi wanaibua hoja hiyo, shahidi hakuwa anatoa ushahidi wake.

“Wakati wanatoa hoja walisema shahidi anaonekana ana vitu pale kwenye kizimba na ana pen ananukuu. Na wakasema ana simu. Wakati hayo yanatokea shahidi alikuwa hatoi ushahidi. Alikuwa amekaa anasikiliza malumbano ya hoja,” amedai Chavula

“Na hata hayo yanayosemwa alikuwa anayafanya, alikuwa hayafanyi. Mheshimiwa Jaji wakati shahidi anaongozwa kuanzia maapisho mpaka anatoa ushahidi wake, Mahakama ilikuwa ikimtizama. Hakuna hata mmoja wetu alisimama kwamba shahidi alikuwa anaongozwa na kuna vitu alikuwa anasoma kuvirejea. Hiyo hoja haikuletwa,” amedai

Aidha, Wakili Chavula amedai, upande wa utetezi haukuonesha mahakamani namna shahidi huyo alivyokuwa anatumia vifaa hivyo akiwa katika kizimba.

“Lakini Mheshimiwa Jaji, hakuna mahala Mahakama yako imeelezwa kwamba wakati akiulizwa maswali na mwendesha mashitaka kwamba shahidi alishindwa kujibu na akawa anafungua makabrasha kutoa majibu. Kwa sababu hayo hayapo na hayajajitokeza, Mahakama yako haiwezi kutumia hiki kifungu cha kumpoka sifa shahidi,” amedai Chavula

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, ameiomba mahakama isikubali pingamizi hilo la upande wa utetezi, akidai kwamba hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa shahidi huyo alivitumia vifaa hivyo wakati akitoa ushahidi.

“Wenzetu hawakatai kwamba kile kilichotokea hapo kizimbani no factual issues. Hilo halina ubishi. Factual issues zinathibitishwa kwa ushahidi katika hoja hii. Factual Issue imetoka nyuma,” amedai

Wakili huyo wa Jamhuri amedai, shahidi alitoa ushahidi wake kwa kutumia uelewa wake.

“Tunawasilisha kwamba alichokuwa anakitokea ushahidi shahidi ni majibu kutoka kwenye uelewa wake na si vinginevyo. Mheshimiwa Jaji, Mahakama yako umealikwa kutumia examination room test. Sisi tunasema siyo sawasawa,” amedai Wakili Hilla na kuongeza:

“Examination Room ina kanuni zake na sheria zake. Test ya kisheria ni Ile iliyopo kwenye section one ya Sheria ya Ushahidi. Wamesema kwamba shahidi amekutwa na unauthorized material, lakini hilo pekee halitoshi kumwondoa au kumtengua shahidi. Haya ni masuala ya kisheria na yanapaswa kufanyika kisheria.

Mawakili wa pande zote wanaendelea kujenga hoja kwenye pingamizi hilo. Endelea kufuatilia MwanAHLISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!