Tuesday , 21 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Mkandarasi afurahia kufanya kazi Zanzibar
Habari Mchanganyiko

Mkandarasi afurahia kufanya kazi Zanzibar

Spread the love

 

MKANDARASI wa CCECC kutoka China amesema wanafurahia kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kuridhishwa na namna walivyopokewa na wananchi wakati huu wakitekeleza mradi wa ujenzi wa barabara itakayokuwa na njia ya juu, ikiwa ni ya kwanza kwa hapa Zanzibar. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Barabara ya juu itakuwepo eneo la makutano ya Mwanakwerekwe mpaka Amani, kuunganisha barabara ya kilomita 100.9 kwa jumla itokayo Kiembesamaki, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) mpaka Mtoni ambako itaunganishwa barabara ya Kinazini-Bububu iliyojengwa miaka ya 1990 na kampuni ya Kajima ya Japan.

Mkurugenzi Mtendaji wa CCECC, Zhang Junle amewaambia waandishi wa habari aliokutana nao leo Jumanne kwenye Hoteli ya Serena mjini hapa, kwamba ushirikiano mzuri husaidia ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema kazi ya ujenzi wa barabara hiyo itakayokamilika mwaka 2025, inaendelea vizuri ikiwa tayari imefikia karibu asilimia 29, licha ya matatizo madogo yanayotokea ikiwemo masafa ya kilomita 25 kufuata kokoto Kibele.

Junle amesema CECC ambayo ni miongoni mwa taasisi zilizo chini ya Idara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya China, inapata msaada wa Serikali Zanzibar na imeanza kushughulikia ulipaji wa fidia kwa wananchi walioguswa na ujenzi wa mradi huo, baada ya kupokea orodha ya wanaostahili kulipwa.

Kiasi cha Sh. 3 Bilioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili hiyo; wakati gharama za ujenzi wa mradi mzima wa kilomita 100.9 ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni Sh. 232 Bilioni ikijumuisha njia ya juu.

“Kwanza tunafurahi kupokewa kwa uchangamfu na wananchi. Tunapata ushirikiano wa karibu sana na Serikali inatupa sapoti kubwa kufanya kazi yetu. Inafurahisha kwa kweli,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa wakandarasi waliokuja kwa mara ya kwanza Zanzibar mwaka 2018 kusaini mkataba wa kujenga barabara ya kilomita 52 ya Bububu-Mkokotoni kupitia Kinyasini na Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini, Unguja.

Kwa sasa wakisubiri malipo ya awali – fedha zinalipwa kwa dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – wanatekekeza mradi wa barabara ambao mkataba wake ulisainiwa Julai 2022, wanaendelea kuwapatia mafunzo wafanyakazi wenyeji wapatao 960 kwenye maeneo tofauti ya ufundi ikiwemo uendeshaji mashine (mitambo), mchundo, wahandisi, wasanifu na usimamizi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema mradi huo unagharimu Sh. 232 Bilioni na kuahidi kuwa njia ya juu eneo la Mwanakwerekwe itakuwa tayari ifikapo Oktoba mwaka huu.

Kampuni ya CCECC (China Civil Engineering Corporation) imepata mikataba ya jumla ya kilomita 235 Zanzibar, zikiwemo zilizoko kisiwani Pemba, baadhi zikiwa mpya na nyengine za kuimarisha.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Hukumu mahakama kuu yabatilishwa kesi State Oil, Equity Bank Tz

Spread the loveMAHAKAMA ya Rufani, jijini Dar es Salaam, imebatilisha hukumu iliyotolewa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Geita, Mwanza waongoza kwa mbwa

Spread the loveNaibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema taarifa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Watumishi 25,039, taasisi 65 wahamia Dodoma

Spread the loveSerikali imesema hadi sasa, jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yapata idhini kuwa wakala wa madalali wa DSE

Spread the loveBenki ya NMB imepata idhini kutoka Benki Kuu ya Tanzania...

error: Content is protected !!