August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Miaka 50 ya STAMICO, miti 10,000 kupandwa

Spread the love

WAKATI Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), likianza maadhimisho ya miaka 50 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1972, jumla ya miti 10,000 inatarajiwa kupandwa nchi nzima huku 100 ikianza kupandwa katika Kata ya Ipagala iliyopo mkoani Dodoma na kuendelea na zoezi hilo katika mikoa mingine nchini. Anaripoti Gabriel Mushi… (endelea).

Zoezi hilo la upandaji miti linalenga kutunza mazingira kulinda uoto wa asili wa nchi na kuungana na nchi nyingine kupambana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

Hayo yameelezwa leo tarehe 2 Agosti, 2022 jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk. Venance Mwasse wakati akizungumzia na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho  ya miaka 50 shirika hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo, Dk.Venace Mwace akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)

Amesema Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Dk. Selemani Jafo ndiye atakayekuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo tarehe 12 Agosti mwaka huu.

Amesema kauli mbiu ya zoezi hilo ni ‘Panda miti, tumia mkaa mbadala na rafiki briquettes kuokoa mazingira.’

“Kutakuwa na uzinduzi wa bidhaa mpya ambayo ni mkaa mbadala ambayo inaitwa rafiki briquettes, tunakuja na nishati mbadala kwa ajili ya matumizi ya majumbani ambapo inaungana na kauli mbiu yetu.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo.

“Tunajua watanzania wengi wanatumia mkaa wa miti na kuni ambayo inasababisha kukata miti, shirika limekuja ubunifu makini ulitokana na utafiti uliuofanywa kwa kushirikisha taasisi nyingine kama vile Costech, Tirdo,” amesema.

Amesema tayari utafiti wa nishati hiyo mbadala umekamilika na tayari mtambo wa kuanza uzalishaji wa majaribio umeingizwa nchini lakini pia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeshatoa cheti kudhibitisha kwamba hiyo ni bidhaa salama kwa watanzania.

“Tunaenda kutoa suluhisho la kudumu katika matumizi ya mkaa badala ya kuendelea kukata miti,” amesema.

Aidha, mbali na zoezi hilo la upandaji miti, pia Dk. Mwace amesema watatoa vifaa vya msaada kwa wachimbaji wadogo wenye usikivu hafifu waliopo katika wilaya ya Mbogwe mkoan Geita.

Meneja Masoko Uhusiano wa Shirika la Madini STAMICO hilo, Geofrey Meena akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye ofisi za shirika hilo Upanga jijini Dar es Salaam leo.

“Tunatoa fursa sawa hata kwa walemavu kwamba nao wavune rasilimali za nchi yao. Yote haya yanaungana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba kunakuwa na uchumi jumuishi usiomuacha yeyote nyuma kwa ustawi wa wote kwa kuwa wao tumeanza nao muda mrefu tumewapa mafunzo, tumewapa vifaa vya awali.

“Lakini miaka 50 ya Stamico haiwaachi nyuma tunaenda kuwapa vifaa ili waendelee kutumia fursa ya madini kujitafutia maisha,” amesema.

Pia amesema kutakuwa na zoezi la kuwatembelea viongozi waliowahi kuongoza shirika hilo pamoja na wengine kwa ajili ya kuwahoji na kuwapa taarifa kuhusu maendeleo ya shirika hilo.

“Pia tutawatembelea wagonjwa hususani wanaosumbuliwa na saratani na kuwapa misaada ya msingi,” amesema.

error: Content is protected !!