August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ufadhili NMB wafikia trilioni 1.56 sekta ya kilimo

Spread the love

SERIKALI imezichagiza benki nchini kuwaongezea wakulima, wafugaji na wavuvi fursa za kukopa ili kuongeza uwekezaji kwenye sekta jumla ya kilimo ili kishamili na kuchangia zaidi juhudi za ujenzi wa Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Hayo yalisemwa jana Jumatatu, tarehe 1 Agosti 2022 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kwenye ufunguzi rasmi wa maonyesho ya mwaka huu ya Nane Nane yanayofanyika kitaifa mkoani Mbeya.

Kiongozi huyo alizipongeza benki kwa kupunguza riba hadi asilimia tisa lakini akazitaka kupunguza kiwango hicho zaidi ili kuwawezesha watu wengi kuweza kukopa.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, wakulima, wafugaji na wavuvi wanahitaji mikopo zaidi ili kuongeza uwekezaji na uzalishaji kwa ajili ya kupunguza changamoto ya ajira nchini.

Aidha, alitabainisha maendeleo ya kilimo yanahitaji ufadhili mkubwa kitu ambacho Benki ya NMB imesema imekuwa ikifanya kwa muda mrefu na kuwekeza zaidi ya TZS trilioni 1.56 katika miaka mitano iliyopita.

Akizungumzia mikopo hiyo, Meneja wa NMB Nyanda za Juu, Stratton Chilongola, amesema ukopeshaji unaofanywa na benki hiyo umekuwa na tija kubwa katika mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.

Mikopo ya NMB, Chilongola alifafanua, imewawezesha wakulima, wavuvi na wafugaji kuchangia ukuaji wa pato la taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Akielezea ufadhili wa NMB kwenye sekta hiyo, alisema mikopo ambayo imetolewa na benki hiyo ni pamoja na zaidi ya Sh 300 bilioni mwaka huu kwa ajili ya kilimo cha kahawa, tumbaku, parachichi, mpunga, ufuta, soya na mahindi.

“Kwa mwaka huu, tumetenga Sh 20 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa maghala vijijini (warehouse) kuondoa upotevu wa mazao yao. Tayari tumeshatoa TZS bilioni 6 kama mikopo ya aina hii tangia Januari hadi leo,” Chilongola alibainisha.

“Lakini pia tumekuwa benki ya kwanza kushusha riba hadi asimilia 9 kwenye sekta mama ya kilimo na ufugaji,” aliongeza.

Aidha Chilongola amesema kuwa ndani ya miaka mine NMB imefungua zaidi ya akaunti 644,034 za wakulima nchi nzima.

Pia kupitia NMB Foundation, benki hiyo imetoa elimu ya fedha na mfunzo ya biashara kwa vyama vya ushirika wa wakulima (AMCOS) 1550 nchi nzima, ili kuwajengea uwezo wa namna bora ya kusimamia mapato yao.

“Tunakuja hapa kwenye maonyesho ya Nane Nane kuendeleza uhusiano wenye manufaa kati yetu na wakulima na wafugaji na wadau wengine wa kilimo ili watumie vizuri fursa zilizopo kwenye soko, kukuza mitaji ya biashara zao hivyo ukuaji wa sekta ya kilimo nchini,” Chilongola alifafanua.

Alisema kimsingi NMB inashiriki maonyesho haya ili kuwaelimisha wakulima kwa lengo la kuhakikisha wanapata mafunzo yatakayowawezesha kutunza fedha zao vizuri na pia kukuza mitaji ya kilimo, na kujua fursa za mikopo ya kilimo zinazopatikana NMB.

Kubwa zaidi, Chilongola alibainisha, ni kuwaonyesha wakulima suluhisho za kifedha zinazotolewa na NMB kama huduma ya MshikoFasta ambapo mkulima kupitia NMB MKONONI anaweza kupata mkopo wa hadi 500,000/- papo hapo bila dhamana yoyote.

“Lakini pia kwa wakulima, tayari tunazo bima za hali ya hewa, bima ya mazao yalioko shambani, bima za moto na wizi (kwa mazao yaliyohifadhiwa) na bima kwa ajili ya vifaa vya kilimo,” aliongeza.

error: Content is protected !!