Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Meya Moshi kutimuliwa, vikao CCM vyaendelea
Habari za Siasa

Meya Moshi kutimuliwa, vikao CCM vyaendelea

Juma Raibu, Meya wa Manispaa ya Moshi Mjini
Spread the love

 

KITI cha umeya wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro kinachokaliwa na Juma Raibu kinazidi kufukuta moto, baada ya kamati ya siasa ya wilaya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupendekeza atimuliwe kwenye nafasi hiyo kwa kudhalilisha chama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Raibu amekuwa na wakati mgumu kwenye nafasi hiyo, kutokana na kuhudhuria hafla ya wapenzi wa jinsia moja (mashoga) mwezi uliopita mjini hapa na leo kamati ya siasa ya mkoa, inakutana kujadili mapendekezo ya kamati hiyo ya siasa ya wilaya.

Sherehe hiyo ya siku ya kuzaliwa ya mmoja wa wapenzi hao, ilifanyika Februari 11 mwaka huu, katika ukumbi wa klabu moja iliyopo kata ya Bondeni mjini hapa, ambako Meya alihudhuria akiwa mgeni rasmi.

Ilielezwa kuwa shoga huyo aliyekuwa na wenzake, walimwalika Meya Juma ili watu hao wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, watambulike kwani wanapata taabu kutambuliwa na mamlaka za Serikali.

Kitendo hicho kilikwaza watu mbalimbali likiwamo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Kilimanjaro, walioiandikia barua CCM, kulaani tukio hilo na kutaka hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya kiongozi huyo.

Mbali na BAKWATA, ndani ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, zilidai kuwa kitendo hicho kimewakasirisha madiwani wengi wa CCM, na kumtaka ajiuzulu ili kulinda heshima ya chama chake na Baraza la Madiwani.

Katika kikao cha maandalizi ya Baraza la Madiwani, la Manispaa hiyo kuliibuka mvutano baada ya baadhi ya madiwani kuhoji uhalali wa Meya kushiriki sherehe hiyo, ambayo ni kinyume na msimamo wa Serikali inayopinga vitendo hivyo.

Kutokana na hilo, Kamati ya Maadili na Siasa ya wilaya ya CCM ilipokea malalamiko hayo na ilikutana Februari 26 mwaka huu ambapo Meya alifika mbele ya Kamati ya Maadili.

Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho aliyezungumza na Raia Mwema alisema: “Kikao cha maadili tulikaa kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana na kile cha siasa tulikaa siku hiyo hiyo kuanzia saa 6:30 mchana hadi saa 9 alasiri.”

Mjumbe huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema, “alipokuja kwenye kikao cha maadili, alisema hadi anafika ukumbini hakujua kama ni sherehe ikihusu mashoga na alikuja kupata taarifa baada ya sherehe kumalizika.

“Kwa hiyo, akaomba radhi na kuomba suala hilo liweze kumalizwa kwani hakujua na kama angejua asingekwenda,” alisema.

Chanzo kilisema, baada ya kikao cha maadili kumalizika, kilikutana cha siasa ambapo, “kikao kilimkuta na hatia na kwa mujibu wa Katiba yetu ya chama, tukapendekeza Meya awe chini ya uangalizi wa miezi 12.

“Lakini, tukapendekeza kwa mamlaka ya uteuzi ambayo ni Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kumvua umeya, kwani kitendo alichofanya amekidhalilisha chama kwa nafasi yake,” alidokeza.

Mapendekezo hayo ya Kamati ya Siasa ya Wilaya yaliwasilishwa kwa kamati ya maadili ya mkoa iliyokutana Alhamisi iliyopita na mmoja wa vyanzo vyetu alisema, “sisi nasi tumebariki mapendekezo ya Kamati ya Siasa ya Wilaya na Kesho (leo) Kamati ya Siasa ya Mkoa inakaa.”

Taarifa kutoka kikao hicho kilichokuwa na wajumbe wanane kati ya 10, baada ya wabunge wawili kukosekana, zilieleza kuwa Katibu wa Wilaya na Katibu Mwenezi walikuwa wakimtetea Meya huyo.

“Sasa kwa kuwa tuko wanane, sita tulikuwa tunapinga kitendo alichokifanywa na wawili, waliokuwa wanambeba na wakati kikao kinaendelea, mmoja alikuwa anawatumia ujumbe madiwani kwamba ‘msaidieni Juma’,” kilidokeza na kuongeza:

“Na sisi ujumbe ukatufikia, tukahoji kwa nini mjumbe wa kikao anaendesha kikao kingine kwa kutuma ujumbe kwa madiwani, tukaona hafai kuendelea, tukamtoa kikaoni na tukabaki saba na sita tulitaka hatua kali zichukuliwe na mmoja aliyebaki akawa upande wa Meya.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!