May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ala kiapo elimu watoto wenye mahitaji maalumu

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake haitakubali mtoto wa Kitanzania akose fursa ya elimu kwa sababu ya kuwa na changamoto za kimaumbile. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ahadi hiyo imetolewa na Rais Samia, leo Jumatatu, tarehe 7 Machi 2022, alipowatembelea wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Sekondari ya Benjamini William Mkapa, jijini Dar es Salaam.

“Hatutakubali mtoto wa Kitanzania akose fursa ya kielimu kwa sababu ya changamoto za kimaumbile. Tutafanya kila tunaloweza na mawaziri wamesema hapa tumetoa fedha nyingi kwa ajili yenu, tutaendelea kujenga mazingira wezeshi ili watoto wote waweze kwenda shule,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema, 2021 Serikali ilifanya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum katika kata 3,785, na kubaini kati ya watoto 59,784 wenye mahitaji maalum ni 28,968 na kwamba wote wameandikishwa shule.

Amesema Serikali imeendelea kujenga uelewa kwa jamii kuhusu utambuzi na uandikishwaji shule wa watoto wenye mahitaji maalumu kwa ngazi zote.

“Serikali imshatumia Sh. 5.9 bilioni kununua vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika elimu msingi, sekondari na vyuo. Serikali imetoa mafunzo ya aina tofauti kwa walimu 3,980 wenye taaluma ya elimu maalum ngazi ya msingi, sekondari na vyuo,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa elimu jumuishi wa 2021/22 hadi 2025/26, pamoja na miongozo mbalimbali ya usimamizi na uendeshaji wa taasisi zinazotoa elimu maalumu na jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Amesema lengo likiwa ni kutekeleza azimio namba nne la malengo ya maendeleo endelevu ya kimataifa, linaloelekeza Serikali kutoa elimu bure kwa watoto wote.

Wakati huo huo, Rais Samia ameahidi kufanyia kazi maombi ya mwanafunzi wakidato cha sita wa shule hiyo, mwenye mahitaji maalumu, Emmanuel Mzena, ikiwemo ya kumfungulia taasisi itakayoitumia kutetea haki za watoto wenye mahitaji hayo.

“Mwanangu Emmanuel ameniambia pamoja na changamoto za maisha nimejitahidi nimesoma mpaka kufikia nilipofikia, nitafanya mwaka huu mtihani wa kidato cha sita, akaniambia sina matumaini ya kupata ajira za Serikali, kwa hivi nilivyo, nakuomba mama nikimaliza kidato cha sita nisomeshe nje na ya pili nifungulie taasisi yangu maalumu lengo laNgu kuwasemea watoto kama mimi waliofichwa majumbani watolewe waje wapate elimu.”

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameahidi kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Mkuu wa shule hiyo, Joseph Deo, ya ujenzi wa mabweni, chumba maalum kwa ajili ya upimaji usikivu wa wanafunzi viziwi na vifaa vya kufundishia wenye mahitaji maalumu.

error: Content is protected !!