Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mdee na wenzake waendelea kuwabana vigogo wa Chadema mahakamani
Habari za SiasaTangulizi

Mdee na wenzake waendelea kuwabana vigogo wa Chadema mahakamani

Spread the love

MAWAKILI wa wabunge viti maalum 19, wakiongozwa na Halima  Mdee, wamendelea kuwahoji maswali hya dodoso wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuhusu kiapo kinzani walichowasilisha mahakamani kujibu malalamiko yao ya kuwafukuza kinyume cha sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Ni katika kesi Na. 36/2022, iliyofunguliwa na wabunge hao katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, dhidi ya Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakiiomba mapitio ya kimahakama ili kubaini kama mchakato uliotumika kuwavua uanachama wa Chadema ni halali au ulikuwa batili.

Leo Jumatatu, tarehe 10 Julai 2023, mbele ya Jaji Cyprian Mkeha,  mawakili wa Mdee na wenzake, wakiongozwa na Wakili Ipilinga Panya, walimhoji maswali ya dodoso Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Ruth Mollel, kuhusu namna chama hicho kilivyowafukuza wabunge hao.

Wakili Panya alimhoji Mollel kwa nini mchakato wa kuwafukuza ndani ya Chadema wabunge hao ulifanyika kwa dharura kiasi cha wahusika kushindwa kupata nafasi ya kujitetea, alijibu akidai hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mdee na wenzake kughushi nyaraka za chama hicho kasha kujipeleka bungeni jijini, kitendo alichodai kuwa ni usaliti.

Mollel alidai Mdee na wenzake ni wakaidi kwa kuwa walipewa nafasi ya kusikilizwa lakini walishindwa kutumia na hata walipopewa nafasi ya kusema chochote katika kikao cha Baraza Kuu la Chadema, kilichoketi Mei 2022, kilichotupa rufaa zao, hawakusimama.

Wakili Panya alimhoji Mollel ni chombo gani chenye mamlaka ya kutangaza uteuzi wa wabunge viti maalum, ambapo alijibu akidai NEC.

Baada ya majibu hayo alimhoji tena ni utaratibu gani unatumika kupinga endapo tume hiyo ikitangaza majina ya uteuzi, amejibu akidai ni utaratibu kama uliofanywa na Chadema, kuwavua uanachama kwa kuwa mtu akiwa hana chama hawezi kuwa mbunge.

Katika hatua nyingine, Wakili Panya alimhoji Mollel, kwa nini kura za wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema, kufanya uamuzi dhidi ya rufaa za wabunge hao kupinga kufukuzwa zilifanyika bila usiri, amejibu akidai kulikuwa na viashiria vya rushwa ndiyo maana wajumbe wakapendekeza kura za wazi zifanyike.

Akiendelea kuhojiwa maswali hayo, Mollel alidai Mdee na wenzake walikipasua chama hicho kutokana na usaliti walioufanya kujipeleka bungeni huku wakijua majina yao hayajagteuliwa na ngazi za chini, kasha kupitishwa na  Kamati Kuu ya Chadema.

Kwa upande wa Wakili Aliko Mwamanenge, alimhoji kwa nini Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, John Mnyika, hawakusaini karatasi zilizokuwa na hadidu rejea za kikao cha kamati kuu kilichowavua uanachama Mdee na wenzake, alijibu akidai hana majibu.

Hata hivyo, Wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu, alimuuliza swali la ufafanuzi kuhusu suala hilo, ambapo Mollel alijibu akidai Mbowe na Mnyika, inawezekana hawakusaini kwa kuwa kikao kilichtakiwa kufanya zoezi hilo hakijafanyika.

Baada ya Mollel kumaliza kuhojiwa na pande zote mbili, Jaji Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 26 Julai 2023, ambapo wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Ahmed Rashid Hamis na Marry Florian Joackim, wataendelea kuhojiwa maswali ya dodoso.

Mbali na Mdee, wabunge wengine waliofungua kesi hiyo ni Cecilia Pareso, Stella Siyao, Naghenjwa Kaboyoka, Esther Matiko, Nusrat Hanje, Ester Bulaya na Hawa Mwaifunga.

Katika kesi hiyo Mdee na wenzake wanapinga kufukuzwa Chadema wakidai hawakupewa nafasi ya kusikilizwa, pia hawakujipeleka bungeni kama inavyodaiwa kwa kuwa uteuzi wao ulikuwa na baraka za chama hicho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kwafukuta kisa chaguzi, Lissu aibua tuhuma nzito

Spread the loveCHAGUZI za kusaka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

error: Content is protected !!