Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko MCT, TEF yamwangukia Rais Samia
Habari MchanganyikoTangulizi

MCT, TEF yamwangukia Rais Samia

Spread the love

 

BARAZA la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeiomba Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, iondoe sheria zote kandamizi zinazoathiri uhuru wa vyombo vya habari. Anaripoti Regina Mkonde, Morogoro…(endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumatatu tarehe 10 Mei 2021, na Katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga, akizungumza katika semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa mtandoni, iliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Mkoani Morogoro.

Mukajanga ametoa ombi hilo, wakati akizungumzia agizo la Rais Samia, alilolitoa hivi karibuni la kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa kutokana na sababu mbalimbali.

Amesema agizo la Rais Samia sio suluhu ya changamoto ya vyombo vya habari kufungiwa na kuminywa visifanye kazi zake kwa uhuru, bali inatakiwa sheria zibadilishwe ili uhuru wa vyombo vya habari uenziwe na viongozi watakaofuata.

“Rais Samia akiapisha makatibu wakuu, aliongelea kidogo suala la uhuru wa habari na aliagiza vyombo vifunguliwe. Hili lina mjadala sababu wengine tulisikia ametamka vyombo vya habari lakini wasaidizi wake wamesema agizo lilihusu vyombo ya habari vya mtandaoni.”

“Kwa sababu ofisi yake haijatoa kauli juu ya tarifa ya wasaidizi wake hao, agizo la kufunguliwa mtandaoni bila shaka hilo ndio sahihi,” amesema Mukajanga

Katibu mtendaji huyo amesema “tunadhani bila kushughulikia sheria zinazoongoza, zinazosimamia na kudhibiti kazi zetu, tatizo halitaweza kuondoka.”

“Kwa nia njema hiyo, anaweza akaamua kama hivyo mfungulieni fulani, lakini kama sheria ipo maana yake kesho anaweza pata tatizo mtu mwingine au yuleyule aliyefunguliwa akapata tatizo kutokana na sheria zile zile,” amesema Mukajanga.

Amesema, “hii inatupeleka wapi, tunadhani hii inaonesha umuhimu kutazama mazingira yetu kwa umuhimu zaidi.”

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, (TEF) Deodatus Balile amesema, mchakato wa mabadiliko ya sheria za mtandaoni umeanza kufanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuwaomba wadau kujitokeza kutoa maoni

Alisema, kauli ya Rais Samia haikusema vyombo vya habari vya mtandaoni, “alisema vyombo vya habari vilivyofungiwa, vifunguliwe” na akagusia suala la kanuni ziwe wazi.

Balile amesema, mkanganyiko ulikuja kwa watendaji wa Rais Samia wamekuwa waking’ang’ana ni vya mtandaoni pekee jambo ambalo linaendeleza mjadala wa agizo hilo la Rais.

“Mchakato wa mabadiliko ya sheria tayari umeanza. Vyombo vya habari mtandaoni tunaomba tushiriki kwani TCRA imeanza, tukatoea mawazo yetu. Lakini, sisi waandishi wa habari, tuonyeshe weledi kidogo katika kuhabarisha umma,” amesema Balile

Jumanne ya tarehe 6 Aprili 2021, Rais Samia alitoa amri ya kuachia huru vyombo vyote vya habari wakati akihutubia baada ya kuwaapisha makatibu, manaibu katibu wakuu na viongozi wa taasisi za umma, Ikulu ya Dar es Salaam.

Rais Samia alisema, wizara ya habari inapaswa kusimamia vyombo vya habari “nasikia kuna vijivyombo vya habari mmevifungia fungia, sijui viji- TV vya mikononi vile, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya serikali.”

“Vifungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunabinya uhuru wa vyombo vya habari, lakini mhakikishe kila mliyempa ruhusu ya kuendesha chombo cha serikali anafuata sheria za serikali na kanuni ziwe wazi, kosa hili adhabu yake ni hii na mnakwenda kwa adhabu mlizoziweka kwenye kanuni,” alisema

Katika kusisitiza hilo, Rais Samia alisema “tusifungie tu kibabe. Wafungulieni lakini tuhakikishe wanafuata kanuni na miongozo ya serikali.”

Baadhi ya vyombo vya habari vilivyofungiwa, futiwa leseni au kunyimwa leseni za uendeshaji ni MwanaHALISI, Mawio, Tanzania Daima, Mseto na televisheni ya mtandaoni ya Kwanza TV.

Awali, Mratibu wa THDRC, Onesmo Ole Ngurumwa alisema, semina hiyo ina lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa mtandaoni ambao ni eneo linalokuwa kwa kasi katika siku za hivi karibuni.

Ole Ngurumwa ambaye kitaaluma ni wakili alisema, kutoka na uwepo wa sheria mbalimbali kandamizi kwa eneo la usimamizi wa vyombo vya habari, wamefungua kesi mahakamani ya kuzipinga.

Amesema, mwisho wa mafunzo hayo ya siku tatu, yatawafanya waandishi wa habari wa mitandoni kuwa na uelewa mpana wa masuala mbalimbali ili waweze kutimiza majukumu yao kwa weledi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mchina wa SGR aburuzwa kortini kwa kumjeruhi Mtanzania, TRC waja juu

Spread the love  RAIA wa China, Zheng Yuan Feng, amefikishwa mahakamani kwa...

Habari Mchanganyiko

Watendaji Kata, Mitaa watakaoshindwa kusimamia usafi kukiona

Spread the love  WATENDAJI wa kata, mitaa na vitongoji na maofisa afya...

Habari Mchanganyiko

Mtia nia urais TLS kukata rufaa kupinga kuenguliwa

Spread the love  MTIA nia ya kugombea Urais wa Chama cha Mawakili...

Habari Mchanganyiko

NBC yazindua kampeni ya mkeka wa ushindi na ATM zake

Spread the loveBENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetangaza uzinduzi wa kampeni...

error: Content is protected !!