May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe aweka kambi Shinyanga

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameendelea na utekelezaji wa operesheni mpya ya chama hicho, iliyozinduliwa hivi karibuni ‘Operesheni Haki’, na sasa amepiga kambi mkoani Shinyanga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga…(endelea).

Leo Jumamosi tarehe 29 Mei 2021, Mbowe na ujumbe wake, wamewasili mkoani Shinyanga, wakitokea jijini Arusha, baada ya kuzindua operesheni hiyo Alhamisi tarehe 27 Mei mwaka huu.

Katika ziara yake hiyo, Mbowe ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya Chadema, Wilaya ya Shinyanga Mjini.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema Taifa

Katika hafla hiyo, Mbowe amewahakikishia wanachama wa Chadema mkoani Shinyanga, kwamba, atahakikisha anatafuta fedha za kukamilisha ujenzi huo, kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024.

Pia, Mbowe amesema Chadema kitaendelea kujenga ofisi zake, katika kanda na mikoa mbalimbali, kwa kuwa chama hicho kinazidi kukua.

“Chama chetu kinaendelea kukua siku hadi siku, Shinyanga hatukuwa na makao makuu ya wilaya bali tumenunua jengo la kanda. Tutaendelea kujenga ofisi hizi kwa kushirikiana na wanachama, tuachangia kwa kuhakikisha linakamilika kabla ya uchaguzi ujao wa 2024 na 2025,” amesema Mbowe.

Mbali na uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi hiyo, Mbowe ataongoza kikao cha Kamati ya Utendaji ya Chadema ya Kanda ya Serengeti, katika ofisi za kanda hiyo zilizoko Shinyanga.

Operesheni Haki inatarajiwa kufanyika kwa muda wa mwezi mmoja na nusu kuanzia siku ilipozinduliwa, ambapo kwa kaunzia, itafanyika katika kanda zote 10 za Chadema, Tanzania Bara na Zanzibar, kisha itashushwa hadi ngazi ya chini.

error: Content is protected !!