May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Walimu wageuza madarasa nyumba za kuishi

Spread the love

 

BAADHI ya walimu katika Shule ya Msingi Mwachambia mkoani Singida, wamelazimika kugeuza madarasa kuwa nyumba za kuishi. Anaripoti Hamisi Mguta, Dar es Salaam…(endelea).

Hayo yamebainika jana tarehe 28 Mei 2021, baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, David Silinde, kuitembelea shule hiyo kukagua matumizi ya fedha Sh. 50 milioni, zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za walimu.

Walimu hao walikumbwa na aza hiyo, baada ya ujenzi wa nyumba za walimu kukwama kufuatia hatua ya aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Msingi Mwachambia, Edward Ighonde, na msaidizi wake, Charles Mtiko, kutafuna sehemu ya fedha ya ujenzi huo.

Kufuatia changamoto hiyo, Silinde aliuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo haraka, ili walimu wapate nyumba za kuishi.

Aidha, Silinde aliutaka uongozi wa halmashauri hiyo, utoe Sh. 5,000,000, inayohitajika kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo uliosimama.

“Hiki kilichofanyika katika shule hii ni aibu kwa serikali na kwa walimu wote nchini, Serikali imeleta fedha tangu Juni 2020. Mwalimu mkuu ndio anaongoza hujuma za mwalimu kutokua na nyumba. Wakati katika shule hii, darasa linatumika kama nyumba ya walimu, ni aibu,” alisema Silinde.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri, alisema waliohusika katika ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa nyumba hizo, wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwemo, aliyekuwa mkuu wa shule hiyo kufikishwa mahakamani.

error: Content is protected !!