Thursday , 7 December 2023
Home Habari Mchanganyiko Maofisa uhamiaji wanne Kigoma mbaroni mauaji ya Enos
Habari MchanganyikoTangulizi

Maofisa uhamiaji wanne Kigoma mbaroni mauaji ya Enos

Spread the love

MAOFISA wanne wa Idara ya Uhamiaji wilayani Kakonko mkoani Kigoma wametiwa mbaroni na jeshi Polisi mkoani humo kwa tuhuma za mauaji ya Enos Elias (20). Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma  …(endelea).

Taarifa za kukamatwa kwa maofisa hao zimethibitishwa na Ofisa wa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Novat Dowson alipozungumza na mwandishi wetu kuhusu mwenendo wa tukio hilo la kutatanisha.

Enos anadaiwa kukamatwa na maofisa wa uhamiaji tarehe 27 Oktoba 2023  baaadaye tarehe 3 Novemba 2023 Jeshi la Polisi liliwajulisha wanafamilia wa kijana huyo kuwa wamegundua kaburi jipya porini.

Familia ya Enos imeeleza kuwa ndugu yao alikamatwa na maofisa wa uhamiaji kwenye geti la Kakonko  na kumpeleka mahabusu ya Polisi  tarehe 27 Oktoba 2023 ambapo siku iliyofuata maofisa hao wa uhamiaji walimuondoa polisi na kuondoka naye .

Dada wa Enos, Angel Elias alisema kuwa kaka yake alikamatwa na uhamiaji kwa kudaiwa kuwa sio raia.

“Tulikuwa shambani na mama tulipigiwa simu na kaka (Enos) akiomba namba za Nida ya Mama na kusema kuwa anateseka.

“Tulipomtafuta tena simu haikupatikana ndipo Tulipowasiliana na kaka yetu  mwengine Leopold Kisondoka aliyekwenda mpaka kituo cha Polisi cha Kakonko bila mafanikio”.alieleza.

Alisema walikwenda Polisi mara kadha kutaka kujua taarifa za ndugu yao ambapo waliporejea tarehe 31 Oktoba 2023 mmoja wa maofisa wa polisi aliwaeleza kuwa ndugu yao alipelekwa hapo na maofisa wa uhamiaji lakini walikuja kumchukua siku iliyofuata tarehe 28 Oktoba.

Angel aliendelea kueleza kuwa siku ya tarehe 3 Novemba 2023 walipigiwa simu wakitakiwa kufika kwenye kituo cha Polisi cha Kakonko ambapo walielezwa kuwa kuna kaburi jipya limebainika kwenye pori la Kichacha umbali wa Kilometa 25 kutoka Kakonko.

Aliendelea kueleza kuwa walifuatana na Polisi mpaka kwenye pori hilo ambapo kaburi hilo lilipofukuliwa mama yao alifanikiwa kuubaini mwili wa mwanawe uliokuwa ushaanza kuharibika.

WANANCHI WAITUPIA LAWAMA UHAMIAJI
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya wananchi wa mkoa huo walisema kuwa tukio hilo limewashangaza kwa kuwa ni kawaida kwa maofisa hao kuwakamata wananchi kwa madai hayo hayo yanayofanana na Enos.

 Julias Massabo aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Muhambwe katika Halmashauri ya Kibondo mkoani Kigoma alisema madai ya maofisa uhamiaji kuwatesa wananchi kwa kisingizio cha uraia yameanza siku nyingi.

“Hili la Enos limefahamika, tujiulize matukio kama hayo yaliyotokea kwenye familia ambazo hazina uwezo kuwa kuwasiliana na viongozi siasa au vyombo vya habari ni wangapi? alihoji Massabo.

 Mmoja wa wakazi wa Kasulu mjini, Albano Mateo naye alisema  manyanyaso wanayofanyiwa na maofisa uhamiaji yanawanyima haki za kuishi kama raia ndani ya nchi yao.

“Maofisa uhamiaji waliwahi kunishusha kwenye geti la Kakonko nikiwa kwenye gari nilikuwa natoka Mwanza kwenye biashara zangu nikerejea nyumbani Kasulu nilikamatwa kwa kudhaniwa kuwa mimi sio raia wa nchi hii” alieleza huku machozi yakimlengalenga.

Albano alisema kuwa maofisa hao walimpekua kisha kumweka mahabusu kwa muda wa saa mbili baada ya kujiridhisha kuwa ni raia ndipo wakamuachia.

 “Lakini wakati huo tayari walishanipotezea muda , walishakwamisha biashara zangu na kunipa gharama nyingine za usafiri” alisema Mateo.

Alidai kuwa matendo yanayofanywa na maofisa uhamiaji wa yanalenga kutafuta fedha kwani kuna ishara za rushwa kwa sababu wanaosumbuliwa zaidi ni wafanyabiashara.

 ZITO ATAKA TUME IUNDWE

Kutokana na hali hiyo, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alilitaka jeshi la Polisi nchini kuunda tume ya makamishina wa jeshi hilo  kuchunguza tukio hilo.

“ACT Wazalendo tunalitaka jeshi la polisi litimize wajibu wake kwa kuchunguza kwa kina kifo hiki na wahusika wafikishwe mahakamani,” alisema Zitto.

 Aidha, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mwanamvua Mrindoko naye ameunda kamati ya watu sita kuchunguza suala hilo na kuipa siku saba kukamilisha kazi hiyo.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Shura ya Maimamu kukata rufaa kupinga Sheikh kufungwa miaka 7

Spread the loveSHURA ya Maimamu Tanzania, inakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu...

BiasharaTangulizi

Bei ya Dizeli, Petroli yashuka

Spread the loveBEI ya mafuta kwa mwezi Disemba, imeshuka kutokana na kupungua...

Habari Mchanganyiko

TMA yaagizwa kutangaza mafanikio yao kikanda, kimataifa

Spread the love  KATIBU Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara ameiagiza...

Habari Mchanganyiko

NMB yasaidia waathirika wa mafuriko, maporomoko Hanang

Spread the loveWaathirika wa maporomoko ya tope Wilayani Hanang, mkoani Manyara, waliopoteza...

error: Content is protected !!