Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mambo yatakayofanywa na SADC chini ya Rais Magufuli
Habari za Siasa

Mambo yatakayofanywa na SADC chini ya Rais Magufuli

Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC akihutubia wajumbe wa mkutano huo
Spread the love

JANA tarehe 18 Agosti 2019 Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi 16 mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ulifungwa rasmi, huku wajumbe walioshiriki mkutano huo wakipitisha maazimio kadhaa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mkutano wa 39 wa SADC ulifanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 17 hadi 18 Agosti mwaka huu, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere  (JNIC) jijini Dar es Salaam.

Siku ya kwanza ya mkutano huo, Rais Magufuli alikabidhiwa uenyekiti wa SADC na mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dk. Hage Geingob ambaye ni Rais wa Namibia. Pia, siku hiyo lugha ya Kiswahili ilitangazwa kuwa miongoni mwa lugha nne rasmi za jumuiya hiyo.

Rais John Magufuli ametaja maazimio yaliyofikiwa na wakuu hao wa nchi, ambayo yatatekelezwa wakati akiwa Mwenyekiti wa SADC.

Miongoni mwa maazimio hayo, ni nchi mwanachama wa jumuiya hiyo kuendelea na utekelezaji wa mkakati na mwongozo wa maendeleo ya viwanda wa SADC wa mwaka 2015 hadi 2063.

Pia, wajumbe wa SADC waliazimia kuendelea na uwekezaji katika sekta ya miundombinu, kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na kuboresha sera za uchumi na fedha za jumuiya hiyo.

Azimio lingine alilotaja Rais Magufuli, ni nchi mwanachama wa SADC kuendelea kufuatilia hali ya usalama katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na sekretarieti ya jumuiya hiyo kuanzisha chombo cha kukabiliana na majanga.

Licha ya maazimio hayo, wajumbe wa SADC walijadili maombi ya nchi ya Burundi kujiunga na SADC na kuitaka sekretarieti ya jumuiya hiyo kuitaarifu serikali ya Burundi taratibu ambazo inatakiwa kukamilisha ili ombi lake la kujiunga liweze kukubaliwa.

Vile vile, Rais Magufuli amesema wajumbe wa SADC wamekubaliana kuendelea kuwasiliana na Jumuiya za Kimataifa ili iiondolee vikwazo nchi ya Zimbabwe.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Magufuli SADC, nchi nne za jumuiya hiyo zinatarajia kufanya uchaguzi ambazo ni Malawi, Botswana, Mauritius na Msumbiji, ambapo amezitakia kheri nchi hizo ili zitekeleze zoezi hilo kwa amani na utulivu.

Rais Magufuli atakuwa mwenyekiti wa SADC katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti mwaka huu mpaka Agosti 2020 ambapo anatarajiwa kukabidhi kijiti hicho kwa Rais wa Msumbiji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!