Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mama Janeth Magufuli, ameonesha njia Ikulu
Habari za SiasaTangulizi

Mama Janeth Magufuli, ameonesha njia Ikulu

Janeth Magufuli
Spread the love

 

JANETH, Mjane wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, amejiandikia historia yake. Haiba yake, haifanani na watangulizi wake, katika nafasi hiyo, Salma Kikwete na Anna Mkapa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mama Janeth (60), ni mwanamke mkimya. Aweza kufananishwa kwa mbali na Mama Maria Nyerere, Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hakuwa anajulikana kabla ya mumewe kuingia kwenye siasa. Alianza kuonekana kwenye majukwa ya kisiasa, Julai mwaka 2015, baada ya Magufuli, kuteuliwa kuwa mgombea urais, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa muda wote wa miaka mitano na miezi mitatu, wakati mumewe alipokuwa madarakani, Mama Janeth hakufanya harakati zozote za kisiasa.

Hayati John Magufuli akiwa na mke wake Janeth

Janeth hakuingia kwenye siasa wakati mumewe alipokuwa mbunge kwa miaka 20; na haonekani kama atajitumbukiza kwenye siasa, baada ya mumewe, Hayati Magufuli kufariki dunia, tarehe 17 Machi 2021.

Ni tofauti na mtangulizi wake, Salma Kikwete, mke wa aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Salma amekuwa akijihusisha na siasa kwa miaka mingi. Alijitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM, kupitia mkoa wake wa Lindi, wakati mumewe akiwa madarakani, kwa miaka kumi 2005-2015.

Yawezekana kuna mahali, Salma alitumia hata madaraka ya mumewe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama na rais, kutimiza malengo yake ya kisiasa.

Mama Salma Kikwete

Baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Salma aliteuliwa na Hayati Rais Magufuli kuwa mbunge. Salma aliteuliwa tarehe 2 Machi 2017.

Kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika 28 Oktoba 2021, Salma alijitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge, jimbo la Mchinga, mkoani Lindi ambako alitangazwa mshindi wa nafasi hiyo.

Janeth Magufuli, kitaaluma ni mwalimu, kama ilivyo kwa Salma Kikwete. Wote wawili wamewahi kufundisha shule ya msingi Mbuyuni, iliyopo eneo la Oysterbay, mkoani Dar es Salaam.
Mama Janeth amefundisha shule hiyo, kwa takribani miaka 17.

Alikuwa akisomesha masomo ya jiografia, tehama na historia. Aliwaga wanafunzi na walimu wenzake wa shule hiyo, tarehe 18 Februari 2016, ili kujiandaa na majukumu ya kuwa mke wa rais.

Mama Anna Mkapa

Wakiwa katika shule hiyo, Mama Salma na Mama Janeth, taarifa zinasema, walikuwa chini ya Mwalimu mkuu, Dorothy Malecela.

Wakati akiwa Ikulu, Mama Janeth hakuanzisha taasisi, kwa kusingizio cha kusaidia jamii. Alikuwa mke wa rais – “First Lady,” kweli kweli na mama wa nyumbani.

Lakini Mama Salma Kikwete, alianzisha taasisi yake iliyoitwa Wanawake na Maendeleo (WAMA), akidai imelenga kuleta maendeleo kwa wanawake.

Hata hivyo, taasisi ya Mama Salma, ilisheheni makada wa chama tawala, na kimsingi ilikuwa kama mali yake binafsi.

WAMA ilipokea michango mbalimbali, kutoka kwa viongozi wa mataifa mengine; na au wake wa viongozi hao, kwa kuwa mumewe alikuwa rais na baadhi ya zawadi zilikuja kwa jina la Ikulu. Yawezekana pia kulikuwapo kwa misamaha ya kodi.

Naye Anna Mkapa, mke wa aliyekuwa rais wa tatu, Hayati Benjamin Mkapa, pamoja na kwamba hakujiingiza moja kwa moja kwenye siasa, lakini aliihusisha na shughuli mbalimbali zilizogusa siasa.

Anna Mkapa aliyekuwa First Lady, kutoka tarehe 23 Novemba 1995 hadi 21 Desemba mwaka 2005), alianzisha taasisi yake, aliyoita EOTF (Fursa Sawa kwa wote).

Mama Maria Nyerere

Lakini hakuna ushahidi wa moja kwa moja, unaonyesha kuwa taasisi hii, ilinufaisha “makundi yote.”

Kinachokumbukwa na wengi, ni kwamba kama ilivyokuwa kwa WAMA, shirika la Mama Mkapa (EOTF), lilitumia majengo ya Ikulu, fenicha za Ikulu, maji ya Ikulu, umeme wa Ikulu na hata bili za simu, zililipwa na fedha za umma.

Aidha, wakati Anna na mumewe, Benjamin Mkapa, walipokuwa Ikulu, walianzisha kampuni iliyopewa jina la ANBEN Limited.

Kampuni ilituhumiwa ndani ya Bunge na baadhi ya wabunge wa chama tawala, kwamba ilijimilikisha mgodi wa Kiwira, ikiungana na kampuni nyingine ya Tanpower, ambayo ilikuwa inamilikiwa na Daniel Yona, aliyekuwa mmoja wa mawaziri katika serikali ya Mkapa.

Mambo yote haya, hayakufanywa na Janeth. Mama huyu alikwenda Ikulu kusaidia mume wake kufanya kazi za umma, siyo kutumia madaraka ya mume wake. Hakika, ameonyesha njia, ni vema wengine wakaiga kutoka kwake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!