Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Malipo yote ardhi sasa kupitia NMB  
Habari Mchanganyiko

Malipo yote ardhi sasa kupitia NMB  

Spread the love

BENKI ya NMB imeingia makubaliano na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, yanayolenga kutanua wigo wa uhamasishaji na ulipaji wa Kodi ya Pango la Ardhi na malipo mengine ya sekta hiyo kupitia huduma za NMB Wakala, NMB Mkononi, NMB Direct na matawi ya benki hiyo kote nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula (kushoto), akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi (Kulia) jinsi ya kufanya malipo ya kodi ya pango la Ardhi na malipo mengine sekta hiyo, wakati wa utambulisho wa ushirikiano wa kikazi baina ya wizara na benki hiyo. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana.

Kupitia ushirikiano huo, matawi ya NMB na mawakala yatatoa huduma ya ukadiriaji wa kodi ya ardhi, tozo na malipo mengineyo ya sekta hiyo, hivyo kuondoa ulazima wa wananchi kwenda katika Ofisi za Ardhi ili kujua wanadaiwa kiasi gani, jukumu ambalo linaendelea kupatikana pia wizarani na katika halmashauri zote.

Makubaliano ya ushirikiano huo yaliingiwa jijini Dar es Salaam jana Jumanne, ambako Waziri mwenye dhamana, Angeline Mabula, alisema anaamini yataenda kuwa chachu ya kufikiwa kwa lengo la wizara la kukusanya Sh. Bil. 250.1 kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, ambapo wamekusanya Sh 71 bilioni tu hadi sasa.

Akizungumza wakati wa kutambulisha ushirikiano huo, Waziri Mabula alisema  ulipaji wa Kodi ya Pango la Ardhi ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 33 cha Sheria ya Ardhi (Sura 113) na kuwa kodi hiyo ni sawa na vyanzo vingine vya mapato ya Serikali kwa maendeleo ya Taifa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula (katikati), akifafanua jambo jijini Dar es Salaam jana juu ya ushirikiano walioingia na Benki ya NMB wa uhamasishaji na ulipaji wa kodi ya pango la Ardhi kupitia Benki ya NMB. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Kodi wizara hiyo, Denis Masami na kulia ni Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi.

“Ushirikiano huu ni fursa sasa ya wananchi kulipa kwa haraka na urahisi, kwani hawalazimiki tena kwenda Ofisi za Ardhi au katika Halmashauri zetu, badala yake huduma hizo zote zinapatikana sasa kupitia matawi ya NMB na Mawakala.

“Ushirikiano huu unalenga pia kuongeza uwanda mpana wa kupeleka huduma karibu kwa wananchi, wakiwemo wanufaika wa msamaha wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyeondoa riba na malimbikizo ya pango la ardhi kwa kipindi cha Julai hadi hadi Desemba 2022.

“Tunakaribia kukimaliza kipindi hicho cha msamaha, mwitikio ni mdogo sana, hivyo tunaamini kupitia ushirikiano huu, wananchi watazitumia siku 10 zilizobaki kuhakikisha wanalipia deni la msingi, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ifikapo Januari 1 hawajalipa,” alisema Mabula.

Kwa upande, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Filbert Mponzi, alibainisha ushirikiano huo ni fursa nyingine kwa benki yake kuthibitisha uimara wao katika makusanyo, kama walivyofanya katika GEPG, ambako wameweka rekodi kubwa za makusanyo ya mapato ya Halmashauri mbalimbali.

Mponzi aliwataka wateja wa NMB kutohangaika kwenda katika Ofisi za Ardhi, badala yake watumie matawi ya benki huyo kufanya makadirio na malipo ya Kondi ya Pango la Ardhi na wale ambao hawatumii huduma za NMB, kujiunga na taasisi hiyo kurahisisha michakato na kunufaika kihuduma.

“Mheshimiwa Waziri ni faraja kwetu kufanya mashirikiano mbalimbali na Serikali, na leo tuko hapa kuthibitisha namna tunavyoweza kushiriki kukusanya mapato ya Serikali. Sisi ni vinara wa makusanyo hayo, ambako malipo mengi yanapitia kwetu na kila mmoja analitambua hili.

“Leo tunakuja hapa kuwakaribisha wateja na Watanzania wote na kuthibitisha kwamba NMB tumejipanga vilivyo kupitia matawi zaidi ya 220 na mawakala zaidi ya 17,000, pamoja na NMB Mkononi na Internet Banking, ambako tutashirikiana na Wizara ya Ardhi kufanikisha makusanyo ya Sekta ya Ardhi,” alisema.

Alisisitiza kuwa NMB iko tayari kwa jukumu hilo muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya Taifa na kwamba NMB imeendelea kujiimarisha katika matumizi ya huduma zilizo chini ya mwamvuli wa Teleza Kidijitali, katika kuleta masuluhisho mbalimbali, hivyo akawasihi wananchi wanaotumia huduma hizo, kuendelea kufurahia.

1 Comment

  • Kwa nini NMB isishindanishwe na mabenki mengine nchini badala ya kuipa NMB tenda hiyo bila ya kutangazwa? Kama tumeruhusu mabenki binafsi nchini kwanini wasipewe nafasi sawa na NMB au CRDB? Bado tuko kwenye mfumo wa chama kimoja, gazeti moja, redio moja na benki moja?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Polisi wakanusha kufanya uzembe ajali iliyouwa mwandishi Ayo Tv

Spread the loveJESHI la Polisi limekanusha tuhuma zilizoibuliwa dhidi yake  kwamba limekawia...

Habari Mchanganyiko

Rais Samia kuzindua gazeti litakalotoa habari za wafanyakazi Tanzania

Spread the loveSHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), liko mbioni kufufua...

Habari Mchanganyiko

GGML yaja na teknolojia za kisasa maonesho ya OSHA Arusha

Spread the loveKATIKA kuelimisha wananchi na washiriki wa maonesho ya usalama na...

Habari Mchanganyiko

GGML, OSHA wawanoa mama lishe 50 kukabiliana na majanga ya moto

Spread the loveKampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na...

error: Content is protected !!