Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli amwangukia Kinana
Habari za SiasaTangulizi

Magufuli amwangukia Kinana

Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM (wakwanza) akitete jambo na Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa chama hicho
Spread the love

JOHN Pombe Magufuli, mwenyekiti wa taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amemuomba katibu mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana, kuendelea na wadhifa huo. Anaripoti Saed Kubenea….(endelea).

Vyanzo vya taarifa kutoka Ikulu jijini Dar es Salaam na Ofisi Kuu ya chama hicho, Lumumba zinasema, Rais Magufuli amelazimika kuchukua hatua hiyo, kufuatia kuwapo kwa hofu ya mgawanyiko ndani ya chama chake.

Mmoja wa watoa taarifa wa MwanaHALISI Online ameeleza mwandishi wa taarifa hii, mwishoni mwa wiki kuwa Rais Magufuli alikutana na Kinana, wiki mbili zilizopita kwa lengo kumshawishi ili kuendelea kubakia katika nafasi hiyo.

Kabla ya mkutano huo wa Ikulu, Kinana alishawahi kunukuliwa na baadhi ya watu wake wa karibu kuwa hayuko tayari kuendelea na wadhifa huo baada ya mkutano mkuu wa wa chama hicho unaofanyika leo na kesho mjini Dodoma.

Aidha, vyombo vya habari vimewahi kuripoti mara kadhaa taarifa kuwa katibu mkuu huyo “amesusa” kwenda ofisini kutokana na kutoridhishwa na namna ya mambo yanavyoendeshwa ndani ya chama chake.

Miongoni mwa yanayotajwa kusababisha Kinana kutofika ofisini, ni kuzunguukwa kwenye uteuzi wa makatibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika ngazi ya mikoa na wilaya.

Uteuzi wa makatibu wa CCM wa ngazi ya mikoa na wilaya, ulifanyika 25 Machi mwaka huu, kipindi ambacho mwanasiasa huyo alikuwa nje ya nchi.

Taarifa kuwa Kinana amekimbia ofisi zilikuja kukolezwa na madai yaliyotolewa kwa waandishi wa habari na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, kuwa chama chake kimeamua kumpumzisha Kinana kwa sababu ya matatizo ya kiafya.

Alisema, “tumempa mapumziko Komredi Kinana ili aweze kuangalia afya yake. Huyu bwana amekuwa mgonjwa kwa kipindi kirefu.”

Amesema, “wakati tunamaliza mkutano mkuu maalumu uliopitisha marekebisho na mabadiliko ya katiba, Ndugu Komrade Kinana alikuwa anafanya yote haya, akiwa mgonjwa. Alifanya haya akiugulia.”

Alisema, “kwa hiyo ikakubalika achukue muda wa kutosha wa kuitazama afya yake nje ya nchi. Tayari amerejea nchini, lakini mgonjwa akitoka hospitali hakimbilii kazini au shambani moja kwa moja, anapumzika ili kuimarisha afya yake.

“Na jana (miezi mitano iliyopita) nimezungumza naye na amenithibitishia kuwa anaendelea vizuri. Anasema, yuko madhubuti kabisa kuliko jana….”

Polepole alitoa kauli hiyo, wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kukagua uhai wa chama chake mkoani mkoani Arusha.

Kinana hajaonekana hadharani tangu kumalizika mkutano mkuu wa chama chake, Machi mwaka huu.

“Nakuambia hivi, Rais Magufuli amekutana na Komredi Kinana, Ikulu jijini Dar es Salaam na kumuomba aendelee kushikilia wadhifa wa katibu mkuu,” kimeeleza chanzo cha taarifa cha MwanaHALISI Online.

Amesema, “lakini Kinana alishindwa kutoa jibu la moja kwa moja kuhusiana na jambo hilo. Aliomba apewa muda zaidi ili atafakari na kushauriana na watu wake wa karibu, ikiwamo familia yake.”

Jingine ambalo linadaiwa kumfanya Kinana kukacha ofisi ya chama hicho, ni kuenguliwa kwenye nafasi ya uwaziri, Nape Nnauye.

Nape alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi kwa miaka minane kwa kile kilichoitwa “mafanikio makubwa,” hadi uteuzi wa katibu mpya uliofanyika miezi michache iliyopita.

MwanaHALISI Oniline limeelezwa na mtoa taarifa wake kuwa Kinana hakufurahishwa na jinsi Nape alivyofutwa kazi.

Rais Magufuli, alimfuta kazi mara moja Nape kwa kile kinachotafsiriwa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa, hatua yake ya “kumgusa Paul Makonda.”

Kuna minong’ono kuwa Kinana hakuridhika na hatua hiyo kwa hoja kwamba itaifanya serikali na chama kupoteza vijana imara waliotumika kwa uadilifu.

Minong’ono hiyo ilitokana na kile kilichoitwa na chama hicho tawala, “uvumi mtupu,” kwamba Kinana alitaka kuitisha mkutano na wanahabari siku moja baada ya Nape kuondolewa kwenye wadhifa huo; kuzuiwa kuzungumza na vyombo vya habari na kutishiwa kwa risasi.

Kinana na Nape walizunguka nchi mara mbili na kufufua CCM na kukiandaa kwa ushindi katika uchaguzi wa 2015.

Kishindo cha taarifa kuwa Kinana alipanga kukutana na waandishi wa habari, kilimlazimisha Rais Magufuli kuzungumza mahali alipokuwa mwanasiasa huyo.

Alisema, Kinana alikuwa amemtuma kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu. Alitoa kauli hiyo, wakati wa kuwaapisha mawaziri wake wawili wapya, Prof. Palamagamba Kabudi na Dk. Harrison Mwakyembe.

Gazeti hili limeshindwa kumpata Kinana kuzungumzia suala hilo. Mara zote simu yake ya mkononi ilijibu, “simu unayopiga haipatikani.”

Hata hivyo, kiongozi mmoja ameliambia gazeti hili kuwa Kinana amekubaliana na mapendekezo ya Rais Magufuli ya kutaka kubaki katika nafasi yake.

“Kwa jinsi hali inavyokwenda, siyo ajabu ukisikia Kinana ameamua kujiuzulu wadhifa wake. Kitakachoelezwa ni sababu za kiafya, lakini ukweli ni kwamba hafurahishwi na mwenendo wa uongozi ndani ya chama chake,” ameeleza.

Katika uteuzi wa makatibu wa mikoa na wilaya wa 25 Machi, chama hicho kilitangaza makatibu wapya wa mikoa 31 na wilaya 155 Tanzania Bara.

“Pamoja na kwamba makatibu hawa wanakuja kufanya kazi kwa na katibu mkuu, lakini wameteulwa bila anayefanya nao kazi kuhusishwa. Jambo hilo ndilo lililomsukuma kuamua kupumzika,” ameeleza kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa chama hicho.

Kati ya makatibu wa mikoa 31, makatibu 20 ni wapya na kati ya makatibu wa wilaya 155, makatibu 76 ni wale ambao hawajahi kuajiriwa na chama hicho.

Polepole aliwambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakati akitangaza orodha ya makatibu hao walioteuliwa, kuwa chama hicho kilizingatia maadili, weledi, jinsia na mpango wa kuachiana vijiti kwa kuzingatia rika.

Mbali na kutoshirikishwa katika uteuzi, inaripotiwa kuwa Kinana analalamikia uteuzi wa makatibu wa mikoa kutofuata katiba ya chama chake.

“Makatibu wa mikoa wanathibitishwa na NEC. Hivyo ndivyo katiba ya chama chetu inavyoeleza. Lakini safari hii, makatibu wa mikoa wametangazwa bila kufuata utaratibu huo,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya CCM aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Kwa mujibu wa Ibara ya 108 (12) ya Katiba ya CCM, toleo la 2005, NEC ndio chombo kikuu cha uteuzi wa makatibu wa mikoa na kwamba sharti uteuzi wao uthibitishwe na chombo hicho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kasekenya aipa Tanroads wiki kukarabati barabara Morogoro

Spread the loveNaibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wiki moja...

Habari za SiasaTangulizi

‘Aliyemtonya’ Lissu kuhusu rushwa arejea madarakani

Spread the loveMwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Tutaendelea kupigania malengo ya afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Tanzania...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NHC yadai bil. 2.1 taasisi za Serikali, Waziri atoa maagizo

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii...

error: Content is protected !!