Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif: Jabali la siasa lililoanguka
Habari za SiasaTangulizi

Maalim Seif: Jabali la siasa lililoanguka

Maalim Seif Sharrif Hamad, Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Spread the love

 

MWAMBA wa kisiasa na vuguvugu la demokrasia barani Afrika, umeanguka rasmi na hauwezi tena kurejea ulingoni. Ni Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Maalim Seif amefariki dunia na huhitimisha safari yake ya miaka 77 ulimwenguni, leo Jumatano, tarehe 17 Februari 2021, saa 5:26 asubuhi, katika hospitali ya taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Akitangaza kifo cha kiongozi huyo, ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema, taratibu za mazishi zitatangazwa baadaye na serikali.

Ametangaza siku saba za maombelezo, Unguja na Pemba na kuongeza, “serikali inaendelea kushauriana na familia ya Maalim Seif na chama chake cha ACT-Wazalendo,” kupanga mipango ya mazishi yake.

Maalim Seif, alikuwa amelazwa katika hospitali ya Muhimbili, tokea 9 Februari 2021, kwa ajili ya matibabu.

Kabla ya kufikishwa Muhimbili, Maalim Seif alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja. Alinukuliwa akisema, alipata maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).

Maalim Seif Sharif Hamad (77), alizaliwa tarehe 22 Oktoba 1943, katika eneo la Nyali, lililopo Mtambwe, wilaya ya Wete, mkoani Pemba.

Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Uondwe, kisha akajiunga na shule ya wavulana ya Wete, kati ya mwaka 1950 hadi 1957.

Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi, Maalim Seif alijiunga na elimu ya sekondari, kati ya mwaka 1958 hadi 1961. Alipata elimu yake hiyo, katika shule ya sekondari ya kumbukumbu ya Mfalme George, iliyoko Unguja.

Aliendelea na masomo yake ya kidato cha tano na sita katika shule hiyo ya mfalme George, kutoka mwaka 1962 hadi1963.

Pamoja na kufaulu vizuri sana masomo yake ya kidato cha sita, Maalim Seif hakujiunga na chuo kikuu kwa sababu serikali ilimtaka afanye kazi serikalini, ili kuziba nafasi za kazi zilizokuwa wazi kufuatia raia wengi wa Uingereza waliokuwa serikalini, kuamua kurejea makwao.

Maalim Seif aliajiriwa kama mwalimu kwa miaka tisa – kutoka mwaka 1964 hadi 1972 – ambapo alifundisha katika shule za Sekondari za Fidel Castro, Pemba na Chuo cha Ualimu cha Lumumba, Unguja.

Alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mwaka 1972 kwa ajili ya masomo ya shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa, Usimamizi wa Umma na Uhusiano wa Kimataifa.

Alihitimu mwaka 1975 na kutunukiwa shahada yake ya kwanza katika eneo hilo.

Maalim Seif alikuwa mmoja wa wanafunzi waliofaulu vizuri sana masomo yake UDSM, kiasi ambacho uongozi wa chuo hicho ulipenda abakie kufundisha, lakini mwenyewe hakupenda kufanya hivyo.

Maalim Seif alianza kujifunza na hata kuingia katika masuala ya uongozi mkubwa wa serikali mwaka 1975, alipoteuliwa kuwa msaidizi binafsi wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe.

Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977, alipoteuliwa kuwa waziri wa elimu wa Zanzibar. Alitumika wadhifa huo, hadi mwaka 1980.
Februari mwaka 1984, Maalim Seif aliteuliwa kuwa waziri Kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar – cheo ambacho majuku yake yanafanana na waziri mkuu – katika utawala wa Rais Ali Hassani Mwinyi.

Alishikilia nafasi ya waziri katika kipindi cha utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi na Idris Abdul Wakil, kati ya mwaka 1984 hadi Januari 1988, alipoondolewa kwenye baraza la mawaziri na baadaye kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa maneno mengine, Maalim Seif alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, kati ya mwaka 1977 hadi 1988.

Ilimchukua miaka 22 baadaye kurejea katika nafasi za juu za uongozi Visiwani. Hii ilikuwa mwaka 2010, aliporejea kama Makamu wa Kwanza Rais wa Zainzibar, akitokea Chama cha Wananchi (CUF). Alihudumu kwenye nafasi hii hadi mwaka 2015.

Ndani ya CCM, Maalim Seif ameshika nafasi mbalimbali, ikiwamo wa Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC), kati ya mwaka 1977 hadi 1988. Kati ya mwaka 1982 hadi 1987 alishikilia nafasi ya Katibu wa NEC, Uchumi na Mipango.

Maalim Seif na wenzake kadhaa, akiwamo Hamad Rashid Mohammed, Sudi Yusuf Mgeni na wengine, walifukuzwa uanachama wa CCM mwaka 1988 baada ya kutofautiana mitazamo, juu hasa juu ya muundo wa Muungano.

Alikuwa mmoja wa waanzilishi wa KAMAHURU – vuguvugu la kudai katiba mpya, pamoja na kuwapo kwa mfumo wa vyama vingi – iliyozaliwa jijini Dar es Salaam, kupitia kongamano la kudai mfumo wa vyama vingi, lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, tarehe 11 na Juni 1991.

Maalim Seif hakuwapo katika kongamano hilo, kutokana na kuzuiwa nyumbani kwake, kisiwani Pemba.

Baada ya kuruhusiwa rasmi kuwapo kwa mfumo wa vyama vingi, KAMAHURU kiliungana na Chama Cha Wananchi (CCW), iliyokuwapo Tanzania Bara na kuunda The Civic United Front (CUF – Chama cha Chama cha Wananchi).

Ndani ya CUF, Maalim Seif, alianza kuongoza kama Makamu Mwenyekiti wa kwanza. Mwenyekiti wake, alikuwa James Mapalala. Alihudumu katika wadhifa huo, hadi mwaka 1999 alipochaguliwa kuwa katibu mkuu.

Kimataifa, Maalim amewahi kushikilia wadhifa mkubwa sana kimataifa kati ya mwaka 1997 ha 2001.

Aliwahi kuwa mwenyekiti wa mkutano mkuu wa nchi zisizowakilishwa na mashirika ya watu – The Unrepresented Nations and Peoples Organization (UNPO).

Katika masuala ya uwakilishi na ubunge, Maalim Seif, hakuwa mgeni katika maeneo hayo. Ni mmoja kati ya Watanzania wachache waliobahatika kupitia nafasi zote za uwakilishi – Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge la Muungano.

Alikuwa mbunge wa Bunge la Muungano, kutoka mwaka 1977 hadi 1982 na kati ya mwaka 1977 hadi 980 na 1984 hadi 1988, amekuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kwa muktadha huu, anafahamu vizuri shughuli za Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi na amepata kuzishiriki vilivyo.

Mbio za Urais:

Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi na kabla ya kuingia kwa mfumo huo, Maalim Seif alikuwa akijitosa katika kinyang’anyiro cha urais Visiwani. Ndani ya CCM aliwahi kugombea kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo, mwaka 1985. Hakushinda.

Katika uchaguzi mkuu wa kwanza ulishirikisha vyama vingi, Oktoba mwaka 1995, Maalim Seif alijitosa katika kinyang’anyiro kupitia chama cha CUF, kupambana na mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour.

Maalim Seif alikosa kuingia Ikulu kwa sababu “ilitangazwa” kuwa amepata asilimia 49.76 ya kura zote dhidi ya Dk. Salmin aliyepata asilimia 50.24.

Pamoja na CUF kupinga matokeo hayo, pia waangalizi wote wa kimataifa walisisitiza kuwa uchaguzi ule ulikuwa “mchafu.”

Mwaka 2000 Maalim Seif alijotosa tena katika mbio za kuingia Ikulu. Lakini hakufanikiwa. Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ilimtangaza aliyekuwa mgombea wa CCM, Amani Abeid Karume, kushinda kwa kupata 67.04 asilimia ya kura, dhidi ya asilimia 32.96 alizopata Maalim Seif.

Kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa mwaka 1995, uchaguzi huu, pia ulikosolewa na waangalizi na baadhi ya wale wa ndani.

Baadhi ya jumuiya za kimataifa waliutaja uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, pamoja na matokeo yake, kama moja ya chaguzi zisizofuata misingi ya kidemokrasia huku ukandamizaji wa vyama vya upinzani hususani CUF ukiwa wazi.

Hakuchoka. Mwaka 2005, Maalim Seif alijitosa tena katika kinyang’anyiro hicho. Akatangazwa kushindwa tena na Rais Amani Karume.

Safari hii. Maalim Seif alitangaziwa kupata asilimia 46.07 ya kura dhidi ya 53.18 alizopata Karume.

Chama cha CUF, kilipinga matokeo haya na ikatangaza kutomtambua Karume kama Rais wa Zanzibar. Waangalizi wa kimataifa wakiwamo wale wa Jumuiya ya Madola na taasisi ya demokrasia ya Marekani, ziliweka wazi kuwa uchaguzi ule haukuwa huru na wa haki.

Maalim Seif alitupa karata ya nne ya kusaka urais wa Zanzibar mwaka 2010. Mara hii, alipambana na Dk. Ali Mohamed Shein, ambapo pia ZEC, ilimtangaza Dk. Shein kuwa mshindi kwa kumzidi Maalim Seif kura 4,471.

Ndiyo kusema kuwa Maalim Seif alipata asilimia 49.1 dhidi ya asilimia 50.1 alizotangazwa kuzipata Dk. Shein. Uchaguzi wa mwaka huo pia ulionekana kuwa na kasoro nyingi.

Mwanasiasa huyo, hakukata tamaa. Alijitosa tena kuwania kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kukabiliana na Dk. Shein.

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, aliamua kuufuta uchaguzi wenyewe na matokeo yake na kisha kuitisha uchaguzi mwingine wa marudio, Maalim Seif alionekana kushinda na chama chake kilipata viti vingi Unguja na Pemba.

Kabla ya Jecha kutangaza kufuta uchaguzi huo na matokeo yake yote, tayari uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW), ulikuwa umefanyika na washindi kukabidhiwa vyeti.

Jecha alidai aliamua kufuta uchaguzi huo na matokeo yake, kutokana na kugubikwa na udanganyifu.

Lakini wakati Jecha akidai hayo, ripoti za waangalizi zilionyesha uchaguzi wa 25 Oktoba, 2015 Visiwani ulikuwa huru. Ripoti ambazo zilidai kuwa uchaguzi ulikuwa huru, ni pamoja na ile iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya (SADEC) na Umoja wa Africa (AU).

Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi – Zanzibar na Muungano – pale matokeo ya mbunge, mwakilishi; na au diwani, yanapotangazwa na mshindi kukabidhiwa cheti chake, basi mamlaka ya kubatilisha chochote, yanabaki mikononi mwa mahakama.

Katika ripoti yake, waangalizi walisema, wameridhika na zoezi zima la uchaguzi wa 25 Oktoba 2015, upigaji kura, kuhesabu na kujumuisha matokeo.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Maalim Seif safari hii aligombea kwa mara ya sita kupitia chama cha ACT-Wazalendo na kutangazwa kushindwa na Dk. Hussein Mwinyi.

Katika kipindi cha uhai wake, alikuwa akidai kuwa hajawahi kushindwa kwenye sanduku la kura, ingawa hajawahi kutangazwa kuwa mshindi.

Maalim Seif aliamua kuachana na chama cha CUF – ambacho alikuwa mmoja wa waasisi wake, kufuatia kutoafuatiana na Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alionekana wazi, kuwa yuko pale kwa maslahi ya kundi fulani.

Maalim Seif amekufa akiwa mwenyekiti wa taifa wa ACT- Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais Visiwani, jambo ambalo limedhihirisha kuwa alikuwa Jabari la kisiasa Afrika, na kwamba kutofautiana kwake na walioko madarakani, hakukuwa kunalenga tumbo lake.

Maalim Seif – wengi walipenda kumuita, Rais wa mioyo ya Wazanzibari – ameondoka ulimwenguni, akiwa amecha alama nyingi. Ameacha mafundisho na ameacha kizazi cha uongozi. Tumuenzi.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!