WAKUU wa Mikoa (RC) na Wilaya (DC) nchini Tanzania, ni miongoni mwa watendaji wa Serikali ambao hawatakiwi kuingia katika vituo vya kupiga, kuhesabu au kujumlishia kura. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)
Marufuku hiyo ipo katika Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020 kilichotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania.
Sehemu ya tatu kifungu cha 3.3 ya kitabu cha maadili, imebainisha mambo manne yasiyotakiwa kufanywa na watendaji wa Serikali wakati wa uchaguzi utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.
Mosi; mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuchanganya ziara za kikazi na shughuli za kiuchaguzi na kutumia vyombo au watendaji wa Serikali katika shughuli za uchaguzi kwa manufaa yao.
Pili; mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa Serikali kuingia katika vituo vya kupigia, kuhesabu au kujumulishia kura.

Isipokuwa kwamba mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa Serikali wanaruhusiwa kuingia katika kituo cha kupigia kura kwa madhumuni ya kupiga kura tu.
Kuhusu hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa NEC, Giveness Aswile amesema, maadili hayo yanapaswa kuzingatiwa na kila mmoja ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika na kumalizika salama.
Amesema, kama kuna mtu anakiuka maadili hayo mathalani wakuu hao wa mikoa na wilaya wataonekana katika chumba cha kuhesabu, kujumulisha na kutangaza matokeo wanaweza kukataa kwa kujaza fomu maalum ambazo zinakuwepo kulalamikia suala hilo.
Tatu; waziri au afisa mwandamizi yeyote wa Serikali kumwita msimamizi wa uchaguzi kwa lengo la kujadili masuala ya uchaguzi kuanzia kipindi cha kampeni mpaka kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Nne; kuanzia kipindi cha kampeni za uchaguzi mpaka kutangazwa kwa matokeo, mawaziri hawaruhusiwi
I; kutangaza katika vyombo vya habari au kwa namna yoyote misaada au ahadi ya aina yoyote
II; kutoa ahadi za shughuli za maendeleo ya jamii kwa mfano, kujenga barabara, kusambaza maji na mambo mengine kama hayo kwa lengo la kuungwa mkono kisiasa
III; kutumia madaraka au rasilimali za Serikali kwa shughuli za kampeni za uchaguzi kwa manufaa ya chama chochote au mgombea yeyote.
Leave a comment